Ni Baraka mfululizo zinazoendelea kutiririka kapuni mwa tiktoker Baba Talisha kufuatia ufanisi mkubwa alioupata katika kusimamia na kuratibu mazishi ya tiktoker mwenza, marehemu Brian Chira.
Siku chache baada ya kuongoza shughuli zote za kumpa heshima za mwisho Chira, Baba Talisha na bintiye wametunukiwa likizo na kampuni ya kitalii ya Expeditions Maasai Safaris ambao wamefadhili likizo yake kwenda Mombasa.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Baba Talisha na bintiye walipakia msururu wa picha na video fupi wakiabiri ndege kuelekea Mombasa, likizo ambayo aliishukuru kampuni ya Expeditions Maasai kwa kumfadhili kwa kila kitu.
Yeye na bintiye kuabiri ndege kwenda Mombasa kwa hisani ya kampuni hiyo ya kusafirisha watalii kunakuja saa chache baada ya kuchapisha video akitunukiwa likizo hiyo.
“Asante Expeditions Maasai Safaris. Wacha Turelax hapa Mombatha 👑🙌🙌,” Baba T aliandika kwenye picha hizo.
Expeditions Maasai Safaris walifadhili likizo ya Baba Talisha na bintiye kwenda Mombasa kwa siku tatu na usiku 2 kujivinjari na kusherehekea msimu huu wa Pasaka baada ya wiki 2 zenye shughuli nyingi ya kushughulikia ratiba za mazishi ya Brian Chira.
Mashabiki wake katika mtandao wa Facebook walimpongeza kwa kuonyesha mfano mwema na uwajibikaji katika matumizi ya pesa zilizochangwa kwa ajili ya safari ya mwisho ya Chira, lakini pia wakaipongeza Expeditions Maasai Safaris kwa kutambua matendo mema na kuyatunuku.
Haya hapa ni baadhi ya maoni hayo;
“Ni vizuri kushuhudia mambo makuu yakitendeka kwa wale ambao wamefanya mambo mema kwa ajili ya wengine. Inamaanisha Yesu anaishi kati yetu. Kristo kweli amefufuka! Jumapili ya ufufuo yenye baraka kwako na familia katika uzuri wa Mombasa🙏” alisema Truphyh Hapisu
“Unastahili. Furahia watu wema,” Wanjiku wa Kibe.
“Pongezi Expeditions Maasai kwa kutambua na kutuza matendo mema, kwa kweli nyinyi ni bora katika sekta ya utalii.” Purity Alividza alisema.
Baba Talisha amekuwa mfano wa kuigwa na wengi baada ya kusimama bega kwa began a nyanyake Chira kuhakikisha hafla ya kumzika imekamilika salama.
Siku moja iliyopita, tiktoker huyo alitoa maelezo kwa kudadavua hesabu jinsi michango ya Zaidi ya milioni 8 ilivyotumika, akifichua kwamba salio kwenye benki ni milioni 7.2 ambazo zitatumika kumsaidia ajuza huyo.