Jose Gatutura, Terence wamfariji Kareh B baada ya kumpoteza mwanawe kwenye ajali ya Easy Coach

Mwanawe Kareh B alipoteza maisha katika ajali iliyotokea Jumatatu usiku katika eneo la Mamboleo, Kaunti ya Kisumu

Muhtasari

•“Mungu akufariji na akupe amani ipitayo akili zote za kibinadamu katika nyakati hizi ngumu,” Jose alimwambia Kareh.

•Mchekeshaji Terence Creative pia alichukua muda kumfariji malkia huyo wa Mugithi kwa maneno ya kutia nguvu.

ameongoza wasanii kumfariji Kareh B baada ya kufiwa na mwanawe Joseph Maruli.
Mwanamuziki Jose Gatutura ameongoza wasanii kumfariji Kareh B baada ya kufiwa na mwanawe Joseph Maruli.
Image: HISANI

Wakenya wa tabaka mbalimbali wakiwemo wasanii maarufu wameendelea kumfariji mwimbaji Mary Wangari Gioche almaarufu Kareh B kufuatia kifo cha mwanawe.

Mwanawe Kareh B mwenye umri wa miaka 17,  Joseph Maduli alipoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea Jumatatu usiku katika eneo la Mamboleo, Kaunti ya Kisumu. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa shule ya upili ya Chavakali Boys waliokuwa wakisafiri nyumbani kwa likizo ya Aprili kutumia basi la Easy Coach lililoanguka kwenye makutano ya Mamboleo.

Staa wa Mugithi Jose Gatutura, ambaye ni mshirika mkuu wa Kareh B katika muziki ni miongoni mwa wasanii ambao wameandika jumbe za kumfariji mwimbaji huyo mrembo.

"Ninasikitika kusikia kuhusu kifo cha mtoto wa Kareh B 'Joseph' ambaye jana (Jumatatu) alihusika katika ajali ya barabarani," Jose Gatutura aliandika kwenye Facebook.

“Mungu akufariji na akupe amani ipitayo akili zote za kibinadamu katika nyakati hizi ngumu,” alimwambia Kareh.

Mchekeshaji Lawrence Macharia almaarufu Terence Creative pia alichukua muda kumfariji malkia huyo wa Mugithi kwa maneno ya kutia nguvu.

"Inasikitisha sana, Mungu achukue udhibiti," alisema.

Mwimbaji Mary Lincoln alisema, "Pole kwa kufiwa. Inatia uchungu ooh Mungu akurehemu."

Mwimbaji Kareh B alizungumza na Citizen TV siku ya Jumanne ambapo alieleza jinsi alivyopata habari kuhusu ajali hiyo kupitia mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia Jumanne. Alisema kuwa yeye pamoja na wazazi wengine  tayari walikuwa wameeleza wasiwasi wao kuhusu wanafunzi hao kusafiri usiku, lakini ndio ulikuwa mpango pekee wa safari ambao shule iliweza kuwaandalia wanafunzi hao.

“Sikupata usingizi. Mwendo wa kati ya saa sita unusu na saa saba usiku, habari kwenye mitandao ya kijamii. Hapo ndo nilipata ujumbe kwamba basi ambayo imeanguka ya Chavakali,” alisema Kareh B.

Mwimbaji huyo alisema alikuja kujua kwamba mwanawe alifariki katika ajali hiyo siku ya Jumanne asubuhi, saa kadhaa baada ya ajali hiyo kutokea.

Alibaini kuwa mwanawe aliaga baada ya wanafunzi wengi waliosafiri kutoka Kisumu hadi Nairobi kufika Nairobi Jumanne asubuhi, lakini mwanawe akakosa kufika.

“Nilianza kujiuliza mbona wangu hajafika. Nikiuliza mmoja wa waalimu ambaye alisema alikuwa kwenye eneo la ajali, ananiambia wale ambao walipata majeraha kidogo walipewa ruhusa ya kupigia wazazi wao wawaambie usiwe na wasiwasi niko hospitalini niko sawa,” alisema.

Wanafunzi wengine wawili waliojeruhiwa vibaya kwenye ajali hiyo wanaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali moja mjini Kisumu wakati wengine 32 waliopata majeraha madogo wakiwa walipata matibabu katika hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga