Kikundi cha wanamuziki wa Gengetone cha Ethic Entertainment wametoa masharti magumu kwa aliyekuwa mmoja wao Rekless ambaye miaka michache iliyopita alijitenga na kiku ndi hicho na kuanza kufanya muziki kwa kujitegemea.
Kikundi hicho ambacho kilikuwa miongoni mwa vikundi vya kwanza kabisa kujulikana kutokana na muziki wa Gengetone kilikuwa na watu wanne wakiwemo, Rekless, Swat, Seska na Zilla.
Baada ya kupata umaarufu na pesa pia, kulitajwa kutokea kutokuelewana kundini, huku Rekless akiwa wa kwanza kujiondoa na kusababisha kundi kusalia kilema.
Hata hivyo, miezi kadhaa baadae, wenzake watatu wamejikusanya na kutangaza kurejea kwenye muziki baada ya kimya cha muda lakini wameweka wazi kwamba hawatomruhusu Rekless kurudi hivi hivi bila kupitia mchakato mgumu wa kurudi.
Wakizungumza kwenye blogu moja hivi majuzi, Swat, Seska na Zilla walisema kwamba Rekless aliwatoka kipindi ambacho alikuwa anategemewa Zaidi kwenye kikundi na hivyo kama anataka kurudi, basi lazima apitie mchakato mgumu ili kukubaliwa kuingia kundini upya.
“[Rekless] wewe ulitutoka halafu unarudi tu, unaona sisi tunasema ukitoka na ukitaka kurudi lazima kuna itifaki ambayo ni lazima utafuata ili kukubaliwa tena. Kwa sababu ni Dhahiri sisi tayari tumesonga mbele bila wewe, halafu umetupata hapa na wewe unakuja labda kwa sababu huko kwingine kumekuwa kubaya, hiyo hutokea,” Ethic walisema.
Wakitolea mfano, walisema kwamba hata mchezaji nguli Zaidi duniani, Lionel Messi akitaka kurudi katika klabu iliyomlea kwa miaka mingi, Barcelona, hawezi kurudi tu hivi eti kisa yeye ni gwiji bali sharti afuate baadhi ya itifaki.
“Si kwa ubaya, hata Messi akiweza taka kurudi Barcelona, kuna masharti lazima yafanyike, anaweza nunuliwa kwa pesa kidogo au nyingi kutegemea na maelewano. Kama [Rekless] ataamua anakuja, tutazungumza kama watu wazima wanne tupate mwafaka,” waliongeza.
Watatu hao walisema kwamba hata hivyo hawana roho nyeusi kwa mwenzao aliyeondoka na hata akirudi kutaka kufanya kolabo nao, wako tayari siku yoyote.
“Sisi hatuna ubaya, sisi tunamuombea tu mazuri, pia yeye vile alitoka alituombea mazuri,” waliongeza.