Director Trevor, mwanzilishi na mmiliki wa media ya mtandaoni ya Kenya Online Media amezua utata katika mtandao wa Instagram baada ya kuomba mapendekezo kuhusu aina ya gari ambalo mashabiki wake wangependa amnunulie mfanyikazi wake mpya Eve Nyaga.
Trevor alipakia msururu wa picha wakiwa pamoja na mrembo huyo ambaye alimtambulisha wiki si nyingi kama mrithi wa kile alichokuwa akifanya Eve Mungai kwenye chaneli yao ya pamoja.
Akiomba pendekezo, Trevor alimtamba Eve Nyaga kama malkia wa KOM na kuomba kutajiwa baadhi ya magari ambayo mashabiki wake wangependa amnunulie kama zawadi ya siku yake ya kuzaliwa.
Eve Nyaga anatarajia kushereheka siku yake ya kuzaliwa baadae mwezi huu wa Aprili.
“Ni mwezi wa Kuzaliwa kwa maliia wetu wa KOM, Pendekeza Chapa ya Gari ambayo Tunapaswa Kumpa kama Zawadi,” Trevor aliomba.
Eve Nyaga alianza kujulikana mnamo Machi 18 2024, alipotambulishwa kama mbadala wa Mungai Eve katika mojawapo ya vyombo vya habari vya kidijitali vilivyofaulu nchini Kenya, Kenya Online Media.
Mkurugenzi Mtendaji wa jukwaa hilo, Director Trevor, alifichua kuwa Nyaga alikuwa akijiunga na jukwaa kama mwenyeji na taswira ya chapa.
“Tunawaletea sura mpya zaidi ya Kenya Online Media, mtangazaji wetu mahiri na taswira ya chapa Eve Nyaga! Jitayarishe kuzama katika kiini cha burudani Eve anapokuletea habari za kipekee na kufafanua hadithi zilizo nyuma ya vichwa vya habari. Kaa tayari kwa safari iliyojaa msisimko, maarifa, na burudani isiyo na kikomo anapoleta shauku na ustadi wake mbele!” Trevor alisema katika taarifa yake.