Bobrisky: Mwanamke wa Nigeria aliyebadili jinsia akamatwa kwa kurusha pesa juu

Anadaiwa kutumia vibaya na kukata noti za naira wakati wa onyesho la kwanza la filamu mjini Lagos

Muhtasari

•Mwanamke aliyebadili jinsia anayefahamika kwa jina la Bobrisky, amekamatwa kwa tuhuma za kutumia vibaya pesa.

•Wanasema "alimwaga" noti, kumaanisha kwamba alizirusha hewani kwa ishara ya kushukuru.

Image: BBC

Mmoja wa watu mashuhuri nchini Nigeria, mwanamke aliyebadili jinsia anayefahamika kwa jina la Bobrisky, amekamatwa kwa tuhuma za kutumia vibaya pesa.

Bobrisky, ambaye jina lake halisi ni Idris Okuneye, anadaiwa kutumia vibaya na kukata noti za naira wakati wa onyesho la kwanza la filamu mjini Lagos, mamlaka iliambia BBC.

Wanasema "alimwaga" noti, kumaanisha kwamba alizirusha hewani kwa ishara ya kushukuru.

Mtindo wa "Kumwaga pesa" aina hiyo kwa kawaida hufanywa katika harusi na sherehe za Nigeria.

Hili kitaalamu ni kosa kwani noti huanguka chini ambapo zinaweza kukanyagwa.

Bobrisky alidaiwa kumwaga pesa katika onyesho la kwanza la Ajakaju, filamu iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mwigizaji na mtayarishaji Eniola Ajao, katika Film One Circle Mall, katika soko kuu la Lagos wilaya ya Lekki mwezi uliopita.

Video za tukio hilo zilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Mtu huyo maarufu, ambaye ana wafuasi zaidi ya milioni tano kwenye Instagram, bado hajatoa maoni.

Msemaji wa Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC) Dele Oyewale aliambia BBC kwamba Bobrisky atashtakiwa mahakamani punde tu uchunguzi utakapokamilika, bila kutoa muda uliopangwa.

Mnamo Februari, mwigizaji Oluwadarasimi Omoseyin alihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kwa kumwaga pesa na kukanyaga noti mpya za naira.