Aliyekuwa meneja wa msanii Stevo Simple Boy, Chingiboy amefunguka kuhusu msanii kutoka Pwani, Nyota Ndogo kudai kwamba anamtafuta Stevo kwa udi na uvumba ili kumpa msaada.
Nyota Ndogo kwa Zaidi ya wiki moja amekuwa akionesha nia yake ya kumsaidia Stevo Simple Boy katika mitandao ya kijamii, akiomba mtu yeyote kumsaidia kupata namba ya msanii huyo.
Hata hivyo, Chingoboy Mstado amefichua kupitia instastory yake kwamba Nyota Ndogo ana namba ya Stevo na anashangaa mbona anakwenda kwenye mitandao ya kijamii kuitafuta namba yake.
Chingiboy kwa upande wake, alihisi Nyota Ndogo anatumia kinachoendelea kuhusu maisha ya Stevo Simple Boy kutafuta kiki, akisema kwamba kana kweli anataka kumsaidia basi amtafute kimya kimya kwani ana namba yake ya simu.
“Nyota Ndogo shikamoo mama, kama unataka kusaidia Stevo naomba tu mtafute binafsi maana uko na namba yake. Nilikuwa naomba uachane na mambo ya kumtafuta mtandaoni kwa vile sisi tuliomsaidia faraghani unasema tulikuwa tunamtesa. Mimi ni shabiki yako mkubwa na nakuheshimu lakini kwanza mtafute Stevo umsaidie kisha baadae utatangaza kwenye media,” Chingiboy alimshauri Nyota Ndogo.
Meneja huyo pia alijibu kauli ya Nyota Ndogo kwamba kipindi Fulani nyuma alipokutana na Stevo kwenye shoo jijini Nairobi alimuona kama mtu anayepitia mateso.
Chingiboy alikanusha dai hilo akisema kwamba Stevo alikuwa amewekwa katika maisha ya kisanii hadi pale mambo yalipokwenda mrama kupelekea yeye kurudi Kibera kutoka makazi alimokuwa akiishi huko Buruburu.
“…unasema tulimtesa, na sijui ulitoa wapi hiyo hadithi kwa sababu Stevo mwenyewe hajatokea aseme hivyo. Halafu pia sijui unazungumzia uongozi upi ulikutana nao kwenye shoo kwa sababu mimi hata sijawahi kutana na wewe tukiwa na Stevo Simple Boy.”
Awali, tuliripoti kuhusu kumbukumbu ya Nyota Ndogo alipokutana na Stevo na kusema kwamba msanii huyo wa ‘Freshi Barida’ alikuwa anaonekana kuongozwa katika kila kitu, kiasi kwamba hakuwa anapewa nafasi ya kukaribiwa na mtu yeyote kumuongelesha.
“Tulipokutana naye kwenye ile show Nairobi nilimuangalia nikamuhurumia sana sababu alikuwa ni kama mtu anayeendeshwa. Yaani anakuwa anacontroliwa…Kwaufupi nahisi anateseka sana… Yaani amesimamiwa ili mtu asimsongelee kumchanua ama kumwambia chochote. Kilio cha msaada ndicho nilichoona kwenye macho yake,” Nyota Ndogo alikumbuka.