"Anataka kununua tuk tuk" Eric Omondi afichua mipango ya Stephen Bhingi baada ya kumchangishia 311k

Alifichua kwamba walimlipa Bhingi kodi ya mwaka mmoja na kumnunulia baadhi ya vitu vya nyumba.

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alifichua kwamba waliweza kukusanya takriban Ksh311,000 kwenye nambari ya Stephen Bhingi.

•Eric aliambatanisha taarifa yake na video ya Bw Bhingi akicheka kwa furaha baada ya kununuliwa kitanda kizuri.

alisaidia kumhamisha Stephen Bhingi
Mchekeshaji Eric Omondi alisaidia kumhamisha Stephen Bhingi
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Ilikuwa tabasamu na furaha kubwa kwa mtayarishaji wa maudhui Stephen Okaka almaarufu Stephen Bhingi baada ya mchekeshaji Eric Omondi kumsaidia kuhama kutoka kwa nyumba ambayo amekuwa akiishi hadi makazi bora.

Eric aliingilia kati baada ya shabiki huyo mkubwa wa muziki wa reggae hivi majuzi kutengeneza video akionyesha jinsi nyumba yake ilivyofurika maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

“Yaani hii Kenya siwezi pumzika hata siku moja.. Someone DM me his number. Huyu tunahamisha leo na tubadilishe maisha yake milele,” Eric alisema baada ya kukumbana na video ya kuhuzunisha ya Stephen Bhingi.

Baadaye, alimtafuta mtayarishaji wa maudhui huyo ambaye anajulikana sana kwa upendo wake mkubwa wa reggae na hali yake ya furaha, na akaanzisha kipindi cha moja kwa moja cha kumchangishia pesa ambapo Wakenya walijitolea kumchangia.

“Tumefika huku kwa Ras Stephen Bhingi. Team sisi kwa sisi tumtoe kwa hii nyumba inafurika kila saa kukinyesha. Hebu tubadilishe stori yake,” Eric aliwaambia wafuasi wake kupitia Instagram siku ya Jumanne.

Baada ya kipindi hicho cha kuchangisha pesa, mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show alifichua kwamba waliweza kukusanya takriban Ksh311,000 kwenye nambari ya Bhingi.

Aliwashukuru wote waliochangia na kufichua kwamba tayari walikuwa wamenunua vitu kwa ajili ya nyumba mpya ya Bhingi baada ya kumsaidia kuhama.

“Ukitoa kidogo zaidi ya unachochukua. Ukirekebisha zaidi kidogo kuliko unavyovunja. Kuna mahali pa Watu kama Wewe," Eric alisema.

Aliongeza, “TEAM SISI KWA SISI MWENYEZI MUNGU AKUINUE GUYS NA AJIBU MAOMBI YENU YOTE. NYINYI NI WALE WATUUUUU!!!,Leo tume duka hapa Thika town.”

Mchekeshaji huyo ambaye tayari ameonyesha nia yake ya kujitosa kwenye siasa alifichua jinsi walliweza kutumia pesa ambazo zilichangwa kwa ajili ya Bhingi, na pia kuwataka wafuasi wake kuendelea kumchangisha fedha zaidi ili aweze kutimiza ndoto yake ya kumiliki tuktuk.

"Tulifanikiwa Kuchangisha 311K kwa Ndugu yetu. Tumemlipia Kodi ya Mwaka Mmoja...Anataka kununua Tuk Tuk. Endelea kumbariki kwenye Nambari yake 0723659106 (JINA: STEPHEN OKAKA),” alisema.

Eric aliambatanisha taarifa yake na video ya Bw Bhingi akicheka kwa furaha baada ya kununuliwa kitanda kizuri kutumia fedha zilizochangwa.