Alhamisi, mitandao ya kijamii ilifurika jumbe za kuwahongera wanandoa Njugush na mkewe Celestine baada ya kuweka wazi biashara yao mpya.
Mcheeshaji Njugush na mkewe walijiingiza mazima katika biashara ya uchukuzi wa umma kwa kuzindua mtatu mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 33.
Katika matatu hiyo, Njugush aliweka picha mbalimbali za watu wake wa karibu wakiwemo familia na marafiki waliomsaidia kufanikisha ndoto hiyo huku pia kwa nje akiiandika jina la mwanawe – Tugi.
Katika mahojiano na SPB Buzz, Njugush alifafanua sababu ambazo zilimvutia katika biashara ya uchukuzi wa umma jijini Nairobi lakini pia akatoa kidokezo cha biashara zingine ambazo anatarajia kuzianzisha baadae baada ya kufanikiwa kwa ile ya matatu.
“Siwezi jua jibu la hilo lakini ukweli ni kwamba hakuna biashara ambayo hatujaribu. Tutaingia pia katika ukulima, huu mwaka hakuna kitu hatutajaribu,” Njugush alieleza.
“Hata hii sacco [Super Metro] ambayo nimeingia si yangu, ni mtu aliketi chini akaianzisha, ninachojarbu kusema ni kwamba zile fursa ambazo mtu ameanzisha tunaweza jaribu kuzitumia kujinufaisha,” aliongeza.
Baada ya kuonesha muonekano wa ndani ya gari hilo, watu makini walibaini kwamba kuliuwa na picha nyingi za watu wa karibu kwa Njugush lakini hawakuweza kuona picha au hata jina la Abel Mutua, rafiki wake wa karibu.
Njugush alieleza sababu zilizomfanya kukwepa kuiweka picha ya Mutua kuwa miongoni mwa picha za watu wake wa karibu ndani ya gari.
“Kuna picha za watu wote isipokuwa Abel, nafikiri kila mtu ambaye picha zao ziko pale walichangia kwa njia moja au nyigine. Mtu tu hajachangia na ndio maana sijamchora kwa njia moja au nyingine, kwa sababu katika hii dunia huwezi fanya vitu peke yako.”
Kando na hilo, Njugush pia alieleza maana ya maneno ambayo yalikuwa yameandikwa kwenye gari hilo, akisema Tugi ni jina la mwanawe lakini pia akaeleza kuhusu ‘Kabati’ – neno lililoonekana katika upande wa mbele.
“Kuhusu jina Kabati, Abel alikuwa ananiingilia kuhusu gari nililokuwa nalo. Kusema ukweli hili gari limetokana na pesa tulizouza TX. Abel alikuwa anaita hilo gari kuwa sio gari ni kabati, na mimi nikasema mawe yale ambayo wananirusha ninayaokota na kuyatumia kujenga,” alieleza.