Rev Lucy Natasha kwa mara ya kwanza ameamua kuzungumzia minon’ono ya mitandaoni kuhusu sababu ya kutokuwa na mtoto licha ya kuolewa miaka miwili iliyopita.
Akizungumza na Oga Obinna, Natasha alizungumzia suala hilo na kusema kwamba lipo mikononi mwa Mungu, akisema kuwa ni Baraka ambayo wote – pamoja na mumewe Nabii Stanley Carmel wamekuwa wakiiombea sana.
“Unajua watoto ni urithi kutoka kwa Mungu, bila shaka tunayo hiyo hamu, tunalo hilo ombi na nafikiri kwamba hiyo itakuwa Baraka yenye thamani Zaidi ambayo Mungu atampa mtu yeyote,” Natasha alisema.
Natasha alisema kwamba huwa anaona fahari ya kuwa mama kwa dadake mdogo ambaye ameolewa na kuwa na watoto wawili.
“Dadangu mdogo ameolewa na amebarikiwa na watoto wawili, kwa kawaida huwa naona furaha na fahari ya kuwa mama katika uzazi wake. Pia mimi ninatazamia na kutamani kwamba siku Moja Mungu atatubariki na uzao wa tumbo, kwa sababu hiyo ni Baraka kutoka kwa Mungu, unaweza ukafanya yawezekanayo lakini upate bado,” aliongeza.
“Sisi tunasubiri kwa Mungu, ningependa kupata watoto 2, wa jinsia yoyote yenye Mungu atatupa.”
Kando na uchu wa watoto, mchungaji Natasha pia alisema kwamba anapenda kujivinjari na moja ya vitu anavyovipenda wakati wake wa mapumziko ni kuendesha farasi.
“Huwa nachukua muda kando na shughuli zangu za huduma, natenga muda wa kupumzika. Kila mtu anahitaji muda kama huo. Mimi nafanya shughuli tofauti kama kuendesha farasi, kusikiliza muziki na vingine,” alisema.
Akizungumzia muziki pendwa, Natasha alisema kwamba anapenda sana jinsi msanii Guardian Angel anavyofanya muziki wake na uchu wa kumtumikia Mungu.
Kuhusu utofauti wa tamaduni kwamba kwa Wahindi mwanamke ndiye analipa mahari, Natasha alisema; "Mimi sijalipa mahari lakini tulifika katika sehemu ya maelewano."