Msanii kutoka upande wa Pwani ya Kenya, Nyota Ndogo ameweka wazi azma yake ya kuwashika mkono wasanii wa rap kutoka sehemu hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Nyota Ndogo alisema kwamba licha ya kuwa msanii wa kizazi cha zamani, bado anatamani kufanya angalau kolabo chache na wasanii wa Hip Hop kutoka Pwani.
“Najua mimi ni zilipendwa lakini nitafurahi nikifanya nyimbo moja na wasanii wa nyumbani Mombasa wa HIP HOP. Kilifi moja kuvuka Likoni moja Mombasa moja tana moja malindi moja.tutatoshea kwa nyimbo moja?” Nyota Ndogo alisema.
Mjasiriamali huyo wa mgahawa wa vyakula aina ya chapati aliwatoa wasiwasi wasanii wa HipHop kuhusu video akisema yuko tayari kutumia hata akiba ya mapato kutoka kwa uuzaji wa chapatti zake kwa ajili ya kurekodi video.
“Tuimbeni tu tumepewa vipaji tusikate tamaa...nitakusanya pesa zangu za chapati tufanye video.”
Nyota Ndogo ni mmoja kati ya wasanii wa kitambo ambao walifana kipindi hicho na wimbo wake ‘Watu na viatu’.
Katika siku za hivi karibuni, Nyota Ndogo amekuwa akipaza sauti kuhusu matatizo yanayomkumba msanii Stevo Simple Boy.
Alisema kwamba alikuwa anatafuta namba ya msanii huyo wa Kibera ili kumshika mkono, akisema kwamba msaada aliokuwa nao ni kumsaidia Stevo kurudi shule angalau kupata elimu ya kujua kusoma na kuandika.