Mwanaharakati wa kibinadamu Eric Omondi asubuhi ya Jumatano amezindua boti ya kutoa msaada wa wokozi kwa waathirika wa mafuriko katika maeneo mbali mbali kaunti ya Nairobi na viunga vyake.
Omondi kupitia ukurasa wake wa Instagram, alionekana akishusha boti kutoka kwa gari dogo na kuiweka kwenye barabara ambazo zimegruzwa na kuwa bahari ndogo.
Mwanaharakati huyo ambaye anasemekana kulenga kujitosa kwenye siasa alisema kwamba majira ya asubuhi ya Jumatano, yeye na timu yake walikuwa tayari wameokoa waathirika wa mafuriko 34, akisema wengine wengi bado wamekwama kwenye paa za nyumba ambazo zilizamishwa ndani ya mafuriko.
“Tumeokoa watu 34 Leo kuanzia 8:30am hadi 11am na bado kuna Mamia Waliokwama na Watoto na Maafa yanaweza Kutokea WAKATI WOWOTE!!! Jana usiku tulimuokoa Mwanamke na Watoto wake 3 katika eneo la Ruiru OJ,” alisema.
Omondi alilaumu serikali kuu na serikali za kaunti husika kwa kutochukua hatua za haraka ili kuwaokoa wananchi kutoka hatari ya mafuriko.
“Serikali ya Kenya Ikimbilie MTO MANGELI ATHI KABLA YA KUCHELEWA!!!.MSIBA KARIBU KUTOKEA!!! Kuna Familia zimekwama kwenye juu ya Paa na muda unakwenda…” alisema.
Mafuriko yanaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali katika kaunti ya Nairobi na kaunti jirani kutokana na mvua nyingi ambazo zimekuwa zikinyesha katika siku za hivi karibuni.
Mamlaka ya hali ya anga ilionya kwamba huenda mvua hizo zikaendelea kunyesha hadi mwezi Juni na kutoa tahadhari kwa wanaoishi kwenye maeneo ya mabonde kuhamia sehemu salama.
Hata hivyo, baadhi wamelaumu uongozi wa kaunti kwa kile wanadai kuwa mafuriko mengi yanachangiwa kutokana na kutokuwepo kwa mitaro ya kupitisha maji chafu.