Mchungaji mwenye utata, Victor Kanyari ameapa kuasi ukapera wake uliodumu kwa takribani miaka 10 akisema kwamba ana matumainimakubwa kupata mke kutoka kwa mtandao wa TikTok.
Katika video moja kutoka kwa mahubiri yake kwenye vipindi vya mubashara katika mtandao huo wa video fupi, Kanyari alisema kwamba awali alikuwa ameoa msanii wa injili Betty Bayo lakini baada ya kutengana, sasa anarudi sokoni na anatafuta mke, si kwingine bali TikTok.
Akizungumzia kuhusu kuoa, Kanyari alisema kuwa hatojali kuhusu kujuana na atakayempata tayari kwa ndoa kwenye mtandao huo.
Alisema mambo ya kuchukua muda kujuana baada ya kupata mtu anayekupenda kwenye mitandao ya kijamii ni ya kizamana, sasa hivi ukipatana na mtu na unahisi mnapendana, nenda nalo!
“Sasa hivi sijaona, nilikuwa nimeona Betty Bayo tukazaa na yeye watoto wawili…Sasa hivi Nataka kuoa tena. Na nitaoa kutoka TikTok. Niamini mimi, nitaoa hapa TikTok. Nitapata mwanamke mzuri kutoka TikTok. Na usiniambie eti lazima watu kujuana, hakuna mambo ya kujuana. Mkipendana mshapendana, mnapelekana mnakotaka kupelekana. Mkiwezana sawa, mkishindwa sawa pia,” mtumishi wa Mungu alisema.
Kanyari alisema kwamba hawezi akakwama kwa ndoa ambayo haoni kama itadumu akitolea mfano jinsi walitengana na mzazi mwenzake, Bayo baada ya kushindwa kuelewana.
“Nikishindwa nakuja hapa TikTok nasema huyu tulishindwa kuelewana na tunaachana hivyo, lakini si eti nikae kwa ndoa nikufie kwa ndoa ndio nifurahishe watu kisa mimi ni mhubiri, hapana. Mimi ndio nitakufa sio Mungu, kwa hiyo nitaambia Mungu umenipa huyu mtu tumeachana ni hvyo.”
Mwanamuziki wa Kigoco aliachana na Kanyari mwaka wa 2015 wakati Jicho Pevu ya KTN ilipomfichua. Ufichuzi huo ulifichua kwamba “mtu wa Mungu” mwenye utata alikuwa akiendesha huduma ghushi ambapo aliwalaghai waumini wengi wa kanisa lake.
Kulingana na Bayo, bado wanawasiliana kwa ajili ya watoto wao, jambo ambalo lilisisitizwa na Kanyari kwenye video hiyo ya TikTok akisema Bayo alimpigia simu kuhusiana na karo la shule kwa mwanao ambayo alidai ni laki 3 na nusu katika shule ya kibinafsi.