Rapa mkongwe wa Kenya Nazizi Hirji ameandika ujumbe wa shukrani kwa watu wengi ambao wamempa sapoti katika kipindi cha zaidi ya miezi minne iliyopita wakati akimuomboleza mwanawe Jazeel Adams.
Nazizi alifiwa na mwanawe wa miaka mitatu mnamo Desemba 25, 2024 kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli moja nchini Tanzania ambako familia yake ilikuwa ikiishi. Amekuwa katika kipindi cha maombolezo makali tangu wakati huo na alianza kuonekana hadharani hivi majuzi tu.
Siku ya Jumamosi , mwimbaji huyo mzaliwa wa pwani alichapisha video yake akiwashukuru watu wote ambao wamesimama naye, waliomtia moyo na kumuonyesha sapoti wakati akimuomboleza mwanawe.
“Habari zenu, najua sijakuwa hapa kwa muda. Lakini nataka tu kumshukuru kila mmoja wenu; mashabiki, familia na marafiki ambao wamekuwepo kwa ajili yangu. Imekuwa safari chungu sana lakini nyie mmekuwa nami katika hayo yote na ninajaribu kurejea,” Nazizi alisema kwenye video hiyo aliyoichapisha kwenye Instagram.
Aliambatanisha video hiyo na taarifa nyingine ndefu iliyoandikwa kushukuru juhudi za familia, marafiki na mashabiki katika kumfariji.
"Nyinyi mmekuwa nguvu zangu, kila mtu kwenye DM zangu kwa miezi 5 iliyopita ninyi ni nguvu yangu. Kwa kila mtu ambaye ametembea nami kila hatua katika maumivu haya yasiyoweza kuvumilika. Ninawapenda nyote,” Nazizi aliandika.
Aliongeza, "Kwa ya wazazi kwenye DM ambao wamepoteza watoto wakitoka kwenye maumivu yao ili kunitia moyo, ninahisi kushikamana na kila mmoja wenu kwa njia ambayo maneno hayawezi kuelezea. Nitatembea nanyi milele. Kwa wazazi wangu na Baba Jaz @therealtanaka asante kwa kuwa nguzo zangu uko imara!”
Msanii huyo pia alimshukuru mtoto wake mkubwa Tafari Firaz ambaye alisema ameendelea kumtia moyo asihuzunike na kumkumbusha kuwa yuko na Mungu.
“Kwa marafiki zangu, dada zangu hasa!! Mnajijua wenyewe; Nimebarikiwa kuwa na mduara huu. Nawapenda. Sijawahi kupewa sapoti kiasi hiki maishani mwangu na hiyo ina maana kubwa kwangu katika wakati ambao ninahisi mateso kwa nafsi yangu, mnanikumbusha naweza kufanya hivyo,” alisema.
Pia alieleza jinsi anavyomkumbuka marehemu mwanawe akisema, “Nakumizz Jaz kila sekunde moja. Nyie ndio sababu ya mimi bado niko hapa. Jah awabariki nyote.”