Mwimbaji maarufu wa Kenya Tanasha Donna amejitokeza kujitetea baada ya Pasta Victor Kanyari kumkejeli hivi majuzi wakati wa kipindi cha moja kwa moja kwenye mtandao wa tiktok.
Huku akiwahutubia wafuasi wake kupitia mtandao huo wa kijamii ambao hivi karibuni amegeuka kuwa jukwaa lake la kutoa mahubiri, pasta huyo aliyezingirwa na utata mwingi alimkosoa mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz akimshutumu kwa kufanyiwa upasuaji ili kufanya midomo yake kuwa mikubwa.
Mchungaji huyo anayeendesha kanisa la Salvation Healing Ministry jijini Nairobi alisema alishindwa kuelewa ni kwa nini Tanasha, miongoni mwa wanawake wengine huchagua kufanyiwa upasuaji ili kupanua baadhi ya sehemu za miili yao.
“Leo nimeona Tanasha Donna. Zamani Tanasha alikuwa na tulips tudogo, saai Tanasha ako na lips kubwa. Nikashindwa kwa nini Tanasha anapenda kuwa na mdogo mkubwa hivi?,” Mchungaji Kanyari alihoji kwenye mtandao wa Tiktok.
Aliendelea kumkosoa mama huyo wa mvulana mmoja akisema, “Niliskia eti alifanyiwa upasuaji na kupanuliwa mdomo wake. Nikasema ‘Hoo, amepanuliwa mdomo wake, asante’.
Sijui kama naweza pata mtu anielezee kwa nini wasichana wanapenda kuwa na mdomo mkubwa na wanapenda kuwa na makalio makubwa, na wanapenda kuwa na matiti kubwa…
Tanasha Donna leo amehakikisha ako na lips kubwa, anapenda lips kubwa. Wanataka hivyo. Tanasha Donna nimemwangalia leo na nikathibitisha mdomo wake ni kubwa.”
Wakati alipokuwa akimjibu mchungaji huyo mwenye utata, mwimbaji Tanasha Donna alimkashifu na kusema kwamba hakuwa na ufahamu wa urembo.
Tanasha aibainisha kuwa midomo yake ilikuwa imevimba kwa siku chache tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa urembo na kueleza kuwa uvimbe haudumu.
"Hii ilikuwa siku ya 2/3 ya kujaza na midomo yangu ilikuwa bado imevimba. Uvimbe umepungua kwa mbali. Fillers pia sio vya kudumu. Jifunzeni kuhusu urembo kabla ya kupayuka," Tanasha Donna aliandika.
Pia alimwomba pasta huyo kuangazia masuala ya kanisa na kuepuka kuingilia mambo yake.