Diana Marua amhakikishia upendo mwanawe wa kulea, Morgan Bahati baada ya tukio la kutisha

Mkewe Bahati alimkumbusha Morgan kuhusu upendo wake mkubwa kwake na akamshukuru Mungu kwa kuwalinda.

Muhtasari

•Diana amemsherehekea mtoto wake wa kulea Morgan Bahati, siku moja tu baada ya kunusurika kwenye tukio la kutisha barabarani.

•Alifichua kwamba alikuwa na watoto wake Morgan, Mueni, Heaven, Majesty na Josh wakati tukio hilo lilipotokea.

Diana Marua na Morgan Bahati.
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu maarufu wa Youtube, Diana Marua amemsherehekea mtoto wake wa kulea Morgan Bahati, siku moja tu baada ya kunusurika kwenye tukio la kutisha barabarani.

Morgan alikuwa pamoja na mke huyo wa mwimbaji Kelvin Bahati pamoja na watoto wengine; Majesty Bahati, Heaven Bahati, Mueni Bahati na Josh walipokwama kwenye Barabara ya Thika baada ya gari lao kupasuka tairi siku ya Jumapili usiku.

Jumatatu jioni, mama huyo wa watoto watatu alimkumbusha Morgan kuhusu upendo wake mkubwa kwake na akamshukuru Mungu kwa kuwalinda.

“Mungu ni mwema. Nakupenda mtoto wangu Morgan Bahati,” Diana aliandika chini ya picha yake nzuri na Morgan aliyoichapisha kwenye Instagram.

Aliambatanisha picha hiyo na wimbo wa Benson Boone ‘Beautiful Things’, ambao alisema ni wimbo anaoupenda zaidi Morgan.

Katika chapisho lingine, Diana Marua alitoa taarifa akisimulia tukio la kutisha alilopitia akiwa na watoto wake kwenye Barabara ya Thika siku ya Jumapili usiku.

Mke huyo wa Bahati alifichua kwamba alikuwa na watoto wake Morgan Bahati, Mueni Bahati, Heaven Bahati, Majesty Bahati na Josh wakati tukio hilo lilipotokea.

Walikuwa wakielekea nyumbani kutoka kujiburudisha kwenye sehemu ya burudani wakati gari lake aina ya Range Rover Vogue  lilipopasuka tairi na kuanza kuyumba na kukosa kudhibitika.

"Siku iliyoanza kama nzuri na watoto Morgan Bahati, Mueni Bahati,Heaven Bahati, Majesty Bahati na Josh iligeuka kuwa Ndoto yangu mbaya zaidi! Shetani alikuwa kazini lakini Malaika wa Mungu  walikuwepo, Kuheshimu Agizo lao la kuwatunza Mabinti & Wana wa Mungu 😭🙏🏼,” Diana Marua aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, "Tulitoka tumetoka nje,  tukiimba nyimbo za kurudi nyumbani, tukipeana motisha juu ya mvua hii kubwa ambayo imekuwa kawaida. Sikujua, tairi lilipasuka na lilikuwa limechakaa hadi kwenye ream. Gari letu lilikuwa likiyumba bila udhibiti.”

Mama huyo wa watoto watatu alifichua jinsi alivyojawa na hofu baada ya kugundua tairi ya gari lake ilikuwa imepasuka kabla ya hatimaye kuweza kupunguza mwendo na kusimama.

Kufuatia tukio hilo, mtayarishaji huyo wa maudhui alitoa shukrani zake kwa Mungu kwa kumlinda yeye na familia yake na mumewe kwa kuwasaidia baada ya tukio hilo.

“Niliingiwa na hofu, mshtuko na kuchanganyikiwa! Nilifanikiwa kupunguza mwendo na kusimama kando ya barabara tu kwa ajali mbaya kutokea dakika tano baadaye, mita chache kutoka kwa gari letu. Mume wangu @bahatikenya alikuja kwa wakati na ninachoweza kusema ni ASANTE MUNGU! HUWA HAFELI🙏🏼🙏🏼🙏🏼 ,” Diana alisema.