Mchungaji Robert Burale amewaonya wazazi dhidi ya kuwadekeza wanao kama njia moja ya kulipiza kwa vitu ambavyo wao walivikosa enzi za utoto wao.
Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii, Burale alisema kwamba anajua wazazi wengi wa kizazi hiki hawakupata nafasi nzuri ya kujivinjari kwa vyakula na vitu vingine vizuri wakati wa utoto wao.
Alisema kwamba hata hivyo, hicho hakifai kuwa kisingizio cha kulipiza hilo kwa kuwafanyia wanao vitu hivyo ili nao wasije kujuta ukubwani kwamba kuna baadhi ya vitu walikosa.
Alisema kwamba familia nyingi za sasa zinalea watoto wanyonge katika jamii ambao hawawezi kustahilimi vishindo vya kimaisha kutokana na jinsi ambavyo wanalelewa na kudekezwa kama yai.
“Ndio najua tulikua hatufurahii weetabix na bacon kila siku ... hii isitufanye kuwalisha watoto wetu kwa soseji, bacon, mapochopocho kila siku ili kufidia ukosefu wetu wakati wa kukua. Hatupaswi kulea watoto wa cerelac...” Robert Burale alisema.
Badala yake, Burale alishauri wazazi wasiweke maisha kuwa rahisi kwa wanao kila wakati kwa kuwanunua vyakula vizuri pindi wanavyovihitaji, akisema kwamba wakati mwingine wanafaa kuwapa kangumu badala ya soseji.
“Watoto wanaokula nyama ya nguruwe kila siku na kuwa na juisi nene iliyokamuliwa ya embe huku wakicheza kwenye iPad. Saa zingine wacha wakule KANGUMU,” Burale aliongeza.
Burale ni mmoja wa watu maarufu katika mitandao ya kijamii ambao wanatengeneza na kukuza maoni kutokana na utathmini wa uzoefu wao kimaisha.
Hivi majuzi, alitoa maoni yao akisema kuwa hafikirii ni jambo sahihi kwa watoto kuitwa kwa jina la mama zao kama jina la ukoo.
Burale alisema kuwa mtoto wa kiume shupavu siku zote anastahili kukumbatia jina la ukoo la baba yake licha ya tofauti baina ya mama na baba.