Mwimbaji wa Nigeria Tiwa Savage anajulikana kama "Queen of Afrobeats" lakini sasa anakishusha kipaza sauti kwa muda ili kuigiza kwa mara ya kwanza katika filamu mpya, Water & Garri.
Filamu inayooneshwa sasa kwenye Amazon Prime inamuonesha mwanadada anayeitwa Aisha, aliyeigizwa na Tiwa Savage, mbunifu mahiri wa mitindo ambaye anarejea nyumbani Nigeria baada ya miaka 10 nchini Marekani.
Ingawa mwimbaji huyo aliyeteuliwa na Grammy amewavutia watu kwa sauti yake nyororo, aliiambia podikasti ya BBC Focus on Africa kwamba uigizaji siku zote ni njia anayotaka kuifuata.
"Ninaheshimu sana waigizaji sasa. Ni saa nyingi na unakuwa mtu mwingine kwa muda mrefu," alisema. Aliiambia BBC haikuwa "rahisi".
Ingawa filamu inaweza kuwa mpya, msukumo unatoka kwa EP yake ya mwaka 2021 ya jina moja. Filamu hiyo hapo awali ilikusudiwa kuwa video inayoambatana na mradi huo, lakini alisema walipoanza kurekodi "ilikuwa nzuri sana" waliamua kuifanya kuwa filamu ndefu.
Nyimbo za filamu zinaangazia nyota wengine wa Nigeria kama vile Olamide na mwimbaji aliyeteuliwa na Grammy Ayra Starr.
"Kuna hisia za furaha unapofikiria maji na garri. Tulikuwa tunakula hivyo sana tulipokuwa tukikua," alisema.
Aliongeza kuwa gari, ambayo muhogo wa kusindika, na maji ni michanganyiko isiyo ya kawaida, lakini yanapochanganywa pamoja hutoa kitu kizuri.