Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi, Gideon Mbuvi almaarufu Mike Sonko amejitolea kumsaidia aliyekuwa mwanahabari wa Citizen TV Kimani Mbugua katika safari yake ya kupata nafuu.
Kulingana na mchekeshaji na mtangazaji wa zamani wa redio Oga Obinna, mwanahabari huyo kijana ambaye amekuwa akipambana na masuala ya kisaikolojia kwa sasa amelazwa katika hospitali ya Mathare ambapo anaendelea kupokea matibabu maalum.
Sonko sasa amejitolea kumhamisha kijana huyo kutoka Hospitali ya Mathare hadi kituo cha marekebisho ya tabia cha Hospitali ya Wanawake ya Mombasa baada ya kushauriana na wazazi wake.
“Kwa kushauriana na wazazi wa Kimani Mbugua, nitalipa bili yake katika Hospitali ya Mathari na kumhamishia hadi katika hospitali ya Mombasa Womens, kituo cha marekebisho ya tabia. Kwa sasa, Conjestina Achieng bado yuko na anaendelea vyema,” Mike Sonko alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Gavana huyo wa zamani alitoa kauli hiyo baada ya kufika kwenye kipindi cha Obinna Live kwa mahojiano ambapo alifahamishwa kuhusu hali ya Kimani Mbugua.
Katika mahojiano hayo, mchekeshaji Obinna alidokeza kwamba wanapanga kumpeleka mwanahabari huyo wa zamani kwenye rehab kwa takriban mwaka mzima.
"Ninaweza kulipa bili huko Mathare kisha tunaweza kumhamishia ambapo Conjestina yuko katika Mombasa Women's Hospital kwa sasa. Kuna wagonjwa hata wanaume huko, ni rehab. Hapo tuna madaktari wa kitaalamu, madaktari wazuri sana. Nitalipa bill ya Mathare na nitamlipia huko,” Sonko alisema.
Aidha, mwanasiasa huyo alijitolea kuwapeleka wazazi wa Kimani kwa likizo jijini Mombasa kwa siku kadhaa ambapo watapata kupumzika baada ya mambo ambayo wamepitia.
Pia alijitolea kusaidia kulipa malimbikizo ya kodi ya nyumba ya mwanahabari mkongwe Eunice Ommolo ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu.