Kutana na Baba Konde! Harmonize amuonyesha babake kwa fahari baada ya uzinduzi wa albamu (+picha)

Babake Harmonize ni Muislamu mwenye msimamo mkali ambaye pia ni mwalimu wa Madrassa.

Muhtasari

•Siku ya Jumapili, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alimuonyesha kwa fahari baba yake mzazi, pengine kama njia ya kumsherehekea.

•Konde Boy alichapisha picha ya mzazi huyo wake na chini yake akaandika “Meet my daddy” (Kutana na baba yangu).

HARMONIZE
HARMONIZE
Image: FAcebook

Kufuatia hafla yenye mafanikio ya uzinduzi wa albamu mnamo Jumamosi usiku, staa wa bongo fleva Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amewasherehekea watu kadhaa ambao wamekuwa nguzo katika maisha yake.

Siku ya Jumapili, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alimuonyesha kwa fahari baba yake mzazi, pengine kama njia ya kumsherehekea.

Kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, alichapisha picha ya mzazi huyo wake wa kiume na chini yake akaandika “Meet my daddy” (Kutana na baba yangu) na kuambatanisha ujumbe huo na emoji ya moyo kuashiria upendo.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Babake Harmonize, Bw Abdul Kahali, hajakuwa kwenye macho ya umma kwa muda mrefu na ameonekana kuwa mbali na vyombo vya habari kwa miaka mingi.

Miaka kadhaa iliyopita, katika wimbo wake wa ‘Never Give Up’, Kondeboy alifunguka kuhusu jinsi baba yake alipinga kazi yake ya muziki wa kidunia.

Msanii huyo tajika alifichua kuwa babake ambaye ni Muislamu mwenye msimamo mkali alimpendelea ajishughulishe na masuala ya dini kuliko muziki wa kidunia.

Huku akiomba radhi katika wimbo huo, Harmonize alisema kuwa huenda ni tatizo alifuata ndoto zake au pengine Mungu alimtaka kufuatilia dini.

Pia alitangaza upendo wake kwa baba yake akisema anajivunia kumwita baba.

Kondeboy pia alisimulia jinsi baba yake alivyomlea kwa mafundisho ya kiroho na alisema hilo lilichangia pakubwa katika kumsaidia kiroho.

Baba yake ni mwalimu wa Madrasa na Harmonize katika mahojiano yaliyopita alisema ana mpango wa kumtimizia ndoto yake ya kufika Mecca.

Mnamo mwaka wa 2019, mwimbaji huyo ambaye wakati huo alikuwa katika Lebo ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz alimzawadia mzazi wake gari jipya la 4X4 SUV.