Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel alitoa ahadi maalum kwa mkewe Esther Musila alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa wikendi.
Bi Musila alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 54 mnamo Jumamosi na Guardian Angel alitumia fursa hiyo kutoa ahadi ya kuwa naye katika maisha yao yote.
Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 alisherehekea mapenzi yao na kuapa kuendelea kumpenda mama huyo wa watoto watatu wakubwa kadri siku zinavyosonga.
“Ninaendelea kukupenda zaidi na zaidi. Unajua watu husema ukiwa na miaka 60, nitakuwa sijui nini.. ambayo ni sawa maana kadiri tunavyokua pamoja ndivyo ninavyozidi kukupenda na nitakupenda mpaka ufikishe miaka mia moja.
Bado nitakupenda vivyo hivyo kwa sababu kwangu sio kuhusu umri wako, kwangu ni kuhusu wewe ni nani kwangu. Mtu ambaye wewe ndiye ni muhimu kwangu kuliko umri wako,” Guardian Angel alimwambia mke wake wakati wa mazungumzo yao ambayo walichapisha kwenye chaneli ya YouTube ya Esther Musila.
Msanii huyo wa nyimbo za injili alimshukuru mke wake kwa kuwa naye maishani na akamwomba aendelee kuwepo na kamwe asiondoke.
Kwa upande wake, Esther Musila alitangaza kuridhika kwake na mpenzi wake na akamhakikishia kwamba hatakwenda popote.
“Hapa sing’oki by the way. Hapa sing’oki kabisa,” Bi Musila alijibu.
Wakati wa mazungumzo hayo, wawili hao walifichua kwamba walipoteza marafiki kadhaa baada ya kuanza kuchumbiana takriban miaka minne iliyopita.
Hata hivyo, walibainisha kuwa hawana majuto yoyote juu ya urafiki ambao ulifikia kikomo wakati huo.
"Nilikuwa nikifikiria kuhusu watu tuliowapoteza, na nikagundua kuwa maishani kuna wakati huwa tunabeba mzigo wa binadamu na kumbe tukitoka katika maisha yetu ndio maisha yetu yanakuwa rahisi," Guardian Angel alimwambia mkewe.
Aliongeza, “Kwangu imekuwa safari laini bila watu hao niliowapoteza. Labda wakati huo ningefikiria, mazee sasa hawa jamaa wakienda... Lakini marafiki niliowapoteza sijutii kuwapoteza. Nadhani niliwapoteza kwa sababu bora, na kwa sababu nzuri."
Bi Musila alibainisha kuwa pia alipoteza marafiki wengi baada ya hatua ya kuchumbiana waliyochukua miaka minne iliyopita.
Mama huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa urafiki fulani si muhimu hasa wakati baadhi ya marafiki wanakosa kuonyesha sapoti.
"Unapokua, na unapotambua aina ya mtu ambaye unataka kuwa, ni muhimu tu kuachana na watu ambao kwanza hawakuungi mkono. Watu wanaofikiri kwamba wanapaswa kuwa hapo, na wamethibitisha kwamba si lazima wawepo. Wakati mwingine unalazimisha uhusiano ambao hauitaji kuwa hapo.
Ninaweza kusema sijasafiri katika nuru kama hii maishani mwangu kwa muda mrefu. Nuru ya kusafiri ni muhimu sana kwa sababu unazingatia zaidi kile ambacho ni muhimu kwako kuliko kuwa katika maisha ya watu wengine ambayo haufanyi athari. Sijutii, nadhani kuwa na mtu mmoja ni nzuri, wewe unatosha. Kuna mengi tunayofanya ambayo huchukua muda wetu mwingi,” Bi Musila alimwambia mumewe.