Mkurugenzi ya Chama cha Hakimiliki ya Muziki Kenya (MCSK) Ezekiel Mutua amesherehekea mapato yake ya kwanza kutoka kwa TikTok.
Mtetezi wa maudhui safi alishiriki msisimko wake hadharani.
Katika mtandao wake wa kijamii, alichapisha picha inayoonyesha kiwango cha KSh 1,374 kutoka TikTok hadi akaunti yake ya PayPal.
Kauli ya Mutua sambamba na picha hiyo ilitangaza kuanza kwa misheni yake ya kusafisha jukwaa hilo kwa maudhui yanayofaa, haswa kwa vijana.
Alionyesha kujitolea kwake kuthibitisha kwamba mtu anaweza kufaulu kwenye TikTok na maudhui ya heshima.
“Saa 10:20 jioni leo, nilitoa pesa yangu ya kwanza kutoka kwa TikTok kupitia akaunti yangu ya PayPal. Safari ya kutakasa TikTok kupitia maudhui safi imeanza kwa dhati.
Natumai kuwa mfano kwamba si lazima maudhui yawe machafu ili kuuza," aliandika.
Mkurugenzi huyo aliongezea kuwa ni hamu yake ya kupata pesa nyingi zaidi kwenye jukwaa hilo kupitia maudhui safi.
"Siku moja, nitachapisha milioni moja hapa kupitia maudhui safi na muhimu kwenye TikTok." aliandika.
Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya kufanya mkutano na mhubiri mwenye utata Victor Kanyari kuhusu mwenendo wake jukwaani katika wiki chache zilizopita.
Ezekiel Mutua alikashifu tabia yake akisema alikuwa akionyesha mfano mbaya kwa vijana kwenye TikTok na wafuasi wake kwa vile ana kanisa.