Mwanahabari wa Standard Group Shadrack Mitty afariki dunia

Marehemu alikuwa mwandishi wa habari mwenye uzoefu aliyeangazia habari za elimu.

Muhtasari

•Alifariki alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Mafundisho, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kutokana na matatizo ya moyo.

Mwanahabari wa Standard Group Shadrack Mitty amefariki dunia
Mwanahabari wa Standard Group Shadrack Mitty amefariki dunia
Image: HISANI

Mwanahabari wa Shirika la Standard Group Shadrack Mitty amefariki alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali moja mjini Kiambu.

Alikuwa mwandishi wa habari mwenye uzoefu aliyeangazia habari za elimu.

Alifariki alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Mafundisho, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) kutokana na matatizo ya moyo.

Aliyekuwa ripota mkuu wa masuala ya Kisiasa katika NTV Kenya, Bw Kennedy Murithi Bundi alimtaja Mitty kuwa rafiki wa kweli na mwanahabari aliyejitolea kwa lugha nyingi.

"Nimechanganyikiwa. Nimepotea. Nimeamshwa na habari za kusikitisha za kufiwa na rafiki yangu mkubwa na mfanyakazi mwenzangu katika uwanja wa uandishi wa habari Shadrack Mitty. Mwanahabari mzuri wa lugha nyingi ambaye tulianza naye QTV kabla ya kuhamia KTN. Naandika nenda vizuri kaka, lakini hii imenipiga sana.Simu yetu ya tarehe 10 Mei sasa inajirudia akilini mwangu, pumzika,” alisema Murithi.

Mitty alianza kufanya kazi katika kampuni ya Nation Media Group na baadaye akajiunga na KTN TV inayomilikiwa na Standard Media Group kabla ya kifo chake cha ghafla.

Alitoka Kabras, Kakamega.