Muigizaji mkongwe wa filamu wa Bongo, Irene Uwoya ambaye kwa sasa ni mchungaji na mmiliki wa kanisa la Friends of God Ministry amesimulia jinsi alifikia hatua ya kupafuta wokovu.
Katika video fupi ambaye ameipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, Uwoya anaeleza kisa ambapo Mungu alimtokea siku moja kwa ajili ya mazungumzo kabla ya kufikia uamuzi wa kuachana na mambo ya kidunia kwa ajili ya kueneza injili.
“Ninachoweza kusema, wakati Mungu ananiita, aliniita mimi, hakufanya conference call, ilikuwa ni mwito ambao ulitoka kwake moja kwa moja kuja kwangu na wala si kupitia kwa mtu mwingine. Ni mimi na yeye ndio tuliongea. Hakukuwa na watu wengine ambao walikuwa kwenye hayo maongezi, au kwenye hayo maono au kwenye huo wito,” Uwoya alisisitiza.
Uwoya alikuwa ananyoosha maelezo kuhusu maswali mengi ambayo yamekuwa yakibubujika kutoka kwa watumizi wa mitandao ya kijamii kuhusu iweje yeye kuasi mambo ya kidunia na kutumbukia mazima kwenye injili hata bila kuonesha ishara na dalili kabla.
Alisisitiza kwamba Mungu wakati anamuita, hakupitia kwa mtu mwingine bali alimfuata yeye moja kwa moja kwa ajili ya maongezi kuhusu kumtumikia yeye.
“Imekuwa maswali ni mengi, mambo ni mengi, kila mtu anaongea la kwake. Ninachoweza kusema ni kwamba Mimi nafuata kile ambacho Mungu ananiambia nifanye, au kile ambaco moyo wangu unasema kutokana na ujumbe ambao naupata. Kwa hiyo kusikiliza ni wewe na kuacha ni wewe, mimi simlazimishi mtu anisikilize, nachofanya ni kufikisha ujumbe ambao nimepewa nifikishe, nafanya kile ambacho Mungu amenituma nifanye, natii amri ya Mungu ambayo ameniagiza nifanye,” Uwoya alisema.
Tazama video hii hapa;