Mcheshi mahiri na mwanaharakati Eric Omondi ametoa wito kwa rais William Ruto, makatibu wa baraza la mawaziri, na wabunge kupunguza mishahara yao kwa mwaka mmoja ili kuonyesha mshikamano wao na wakenya wanaokabiliana na gharama kubwa ya maisha.
Katika mahojiano na runinga ya Citizen siku ya Jumatano, Omondi alihimiza rais kupunguza safari zake za usafiri, akisema rasilimali nyingi zinazotumika zinaweza kuelekezwa katika kupunguza gharama ya maisha kwa raia.
"Rais amesafiri mara 68 katika muda wa miezi sita, mara nyingi akiwa na ujumbe mkubwa. Nimemwomba rais apunguze safari zake kwa kiduchu. Sina uhakika ni kwa kiasi gani ombi hili litazingatiwa," Omondi alisema.
"Natoa changamoto kwa serikali - kuanzia rais na naibu rais hadi makatibu wa baraza la mawaziri, makatibu wakuu na wabunge - kupunguza mishahara yao kwa mwaka mmoja," aliongeza.
Omondi alibainisha kuwa baadhi ya safari za nje za rais zina faida ndogo kwa nchi na alipendekeza kutuma wawakilishi kuwa mbadala wenye gharama nafuu.
"Msaada wa kifedha kutoka kwa Joe Biden baada ya ziara ya Ruto haulingani na gharama zilizotumika katika safari hiyo, ikiwa ni pamoja na ndege iliyotumika. Ni lazima tuwajibishe serikali hii," alisisitiza.
"Rais anaposafiri, ujumbe ni mkubwa. Hahitaji kukubali kila mwaliko, hasa kwa kuwa ni pesa za walipa kodi ndizo zinazotumika," Omondi aliongeza.
"Tunapaswa kuweka vipaumbele vyetu sawa ili kutambua ni wapi tunaweza kupunguza matumizi na kuwekeza zaidi katika maendeleo," alisema Omondi.
Fauka ya hayo, alisisitiza umuhimu wa viongozi kuonyesha mfano kwa kupunguza matumizi yao na kuelekeza rasilimali hizo kwa miradi itakayosaidia wananchi moja kwa moja.