Mpenzi wa mtangazaji Betty Kyallo, Charlie, amekanusha madai ya kuwa na umri wa miaka 21 kama inavyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika taarifa aliyowaandikia wakosoaji, kijana huyo alijigamba kuhusu kuwa mtu mwenye furaha baada ya kupata mapenzi kwa mama huyo wa binti mmoja.
Pia aliweka wazi kuwa ana umri wa miaka 26 na sio 21 kama inavyodaiwa.
"Kama mtu wa zamani mwenye huzuni, naweza kusema kwa fahari sihusiani tena na nyinyi watu wasio na furaha wasio na chochote ila chuki. Mwanaume hawezi kupata upendo? Nilipata furaha,” Charlie alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Aliongeza, “Kwa hiyo nyinyi nyote fanyeni hesabu na kututazama tunavyofanya namba. Ben 10 mwenye umri wa miaka 21 ana miaka 26."
Kauli hiyo imekuja huku kijana huyo na Betty Kyallo wakifanya karamu kubwa ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa mnamo Ijumaa usiku. Pia alijivunia kutumia zaidi ya shilingi 300,000 kujiburudisha katika jumba la burudani maarufu jijini Nairobi.
Siku ya Ijumaa, Betty alimfichua mpenzi wake mpya kwa ulimwengu baada ya muda mrefu wa tuhuma na uvumi kutoka kwa wanamtandao. Kufuatia hatua yake, watumiaji wa mitandao ya kijamii waliweza kugundua tofauti ya umri inayoonekana kati ya wapenzi hao wawili huku mtangazaji huyo wa TV akionekana kuwa na umri mkubwa kuliko mpenzi wake Charlie, hii iliibua ukosoaji kutoka kwa sehemu ya watumiaji wa mtandao.
Huku akimtetea siku ya Ijumaa, mwanasosholaiti Vera Sidika alibainisha kuwa wanamtandao bado walimkosoa Betty alipokuwa akichumbiana na wanaume wenye umri mkubwa katika siku za nyuma. Kufuatia hilo, aliwataka watu wakome kumshambulia mama huyo wa binti mmoja na kumwacha afurahie uhusiano wake kwa amani.
“Mpeeni Betty mapumziko. Alipotoka kimapenzi na wanaume wakubwa wote mlikuwa bize kusema aibu kwake kwa kutoka na wababa na wanaume waliooa. Sasa kuchumbiana na kijana ni shida, eeh binadamu!! Acheni msichana afurahi," Vera alisema.
Katika ujumbe wake kwa mpenzi wake usiku wa kuamkia Ijumaa, Betty Kyallo alimtakia mambo mema na kwa uhusiano wao.
"Heri ya kuzaliwa mpenzi. Vicheko zaidi, furaha zaidi, kukumbatiana zaidi, watoto zaidi, sisi zaidi. Ni hivi,” Betty Kyallo aliandika kwenye mtandao wa Instagram.
Aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri yake na mwanaume huyo. Pichani, mwanamume huyo anaonekana kuwa mrefu zaidi na ana rasta kichwani.
Mama huyo wa binti mmoja aliendelea kumshukuru mpenzi wake na kusherehekea mapenzi yao.
"Asante kwa kila kitu. Heri ya kuzaliwa,” aliandika.
Kyallo alijigamba kwa kujipatia mwanamume anayefaa na kuwapuuza kila mtu mwingine.
“Mungu alinitumia aliye sahihi. Nyinyi nyote mnaweza kuwa na hasira,” alisema.
Pia alijigamba kuhusu kuwa na furaha na mpenzi wake mpya na kumtakia mwanaume huyo mafanikio zaidi.
"Naomba mtu wangu ashinde kila wakati. Anashinda lakini nataka ashinde mengi zaidi. Juu ya Mungu. Furaha mke, maisha ya furaha,” alisema.