Staa wa Ohangla Prince Indah aliingia katika hali ya majonzi baada ya mmoja wa wafanyakazi wake na mashabiki watatu kufariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Jumamosi asubuhi.
Prince Indah alithibitisha ajali hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii akifichua kuwa ilitokea katika barabara kuu ya Kisii-Migori mwendo wa saa kumi asubuhi ya Jumamosi.
Aliripoti kwamba ilitokea baada ya gari ambalo linashukiwa kupoteza mwelekeo kutokana na matatizo ya breki kugonga magari yaliyokuwa yameegeshwa mbele ya jumba moja la burudani ambako alikuwa akitumbuiza Ijumaa usiku. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya baadhi ya watu waliofariki papo hapo.
"Rambirambi zangu za dhati ziende kwa familia ya marehemu miongoni mwao wakiwa 3 kati ya mashabiki wangu wanaojulikana na 1 wa wafanyikazi wa @malaikamusicals, utambulisho wa kazi kama mlinzi anayejulikana kwa jina GEORGE OKUL," Prince Indah aliomboleza siku ya Jumamosi.
Pia aliripoti kuwa baadhi ya washiriki wa bendi yake na wafanyakazi wengine walipata majeraha katika ajali hiyo.
“Wana bendi wengine waliopata majeraha makubwa lakini kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri na kutoka hatarini ni DEREVA wa lori ambalo hubeba mitambo yangu ya sauti, amekatwa kichwani, MARCYL ABOGE pia sehemu ya ulinzi wangu ilikatwa kichwa chake, OWEN MUSILA mpiga saksafoni alikuwa amekatwa sana mdomoni,” akasema.
Kufuatia kisa hicho cha kusikitisha, mwimbaji huyo maarufu alitangaza kuwa pesa ambazo zingepatikana kutoka kwa shoo yake katika kaunti ya Siaya Jumamosi usiku zingetumika kulipa bili za hospitali kwa watu walioathiriwa.
Katika taarifa yake, aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuwawezesha kupata fedha za bili za hospitali.