Maandamano ya jana ya kupinga Mswada wa Kifedha wa Mwaka 2024 yalipamba moto huku wasanii mbalimbali wakijitokeza mitaani wakisimama kidete na wananchi wenzao ili kuupinga mswada huo.
Hatua hii ilisaidia mno waandamanaji kwani wasanii hawa waliisaidia kaumu ya watu katika kwa kuwapa motisha kupitia nyimbo na mashairi.Baadhi ya wasanii waliosimama kidete na kujitokeza ni kama ifuatavyo:
King Kaka na Nana Owiti:Waliwasili kwenye maandamano hayo, wakitangamana na mashabiki wao na kupinga vikali mswada huo.
King Kaka alisema kuwa alirejea nchini na alihisi kuwa ni wajibu wake kuungana na wenzake katika kupigania haki zao.
Kate Actress: Licha ya kukumbana na ukosoaji mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kwa maoni yake ya awali, Kate alishiriki maandamano hayo akiwa ameuficha uso wake.
Idadi ya wafuasi wake kwenye Instagram ilipungua, labda kutokana na maoni yake kwamba hakuhitaji pesa za serikali ndipo asonge.
Austin Muigai: Mchekeshaji mahiri aliibeba bendera ya Kenya huku akionekana kuwasaidia vijana kwa kuwapa maji na motisha kupitia nyimbo za maandamano.
Mcheza Santuri Grauchi: Mcheza santuri Grauchi alifanya maandamano kuwa sherehe kwa kuleta gari la kuchezea muziki na kucheza nyimbo kama 'Njege Masanse' ya Wakadinali, ambayo iliwapa nguvu waandamanaji.
Tipsy Gee: Nyota wa muziki wa aina ya Arbantone, maarufu kwa wimbo wake wa 'Kufinish Kumalo,' alionekana katika eneo la CBD licha ya kuathiriwa na gesi ya vitoamachozi. Alijitahidi kupinga mswada wa fedha ambao wengi wanauona kuwa ni adhabu.
Mchekeshaji Mulamwah: Aliwashangaza waandamanaji kwa kuwapa chai kwa mandazi ili kuongeza nguvu zao walipokuwa wakijaribu kufika Bungeni.
Octopizzo: Rapa maarufu anayejulikana kwa asili yake katika mtaa wa Kibera, alijitokeza na walinzi wake, wakiwa tayari kumlinda. Alikuwa amevalia minyororo na alionekana mwenye heshima.
Fauka ya hayo, wasanii wengi chipukizi walijitokeza huku wengi wakibeba mabango ya kuonyesha ghadhabu zao dhidi ya mswada huo. Wengine walitumia fursa hiyo katika kupiga picha ili kupasha ujumbe maalum kwa viongozi wao.