Kwa mara ya kwanza nchini Kenya, mandamano yaliyoandaliwa na vijana wa Gen Z yalivutia watu kutoka matabaka mbalimbali.
Maandamano hayo yalivutia waigizaji, watu maarufu na hata baadhi ya watoto wa wanasiasa ambao walijitokeza kujumuika na vijana wenzao kupinga mswada tata wa fedha wa mwaka 2024, ambao sasa umetupiliwa mbali na rais.
Mmoja wa watu maarufu waliojiokeza kushiriki maandamano hayo ya Amani ambayo yalishuhudia rabsha kutoka kwa polisi kutupa vitoza machozi ni muigizaji Jackie Matubia.
Akizungumza kiini cha yeye kushiriki maandamano, Matubia alisema kuwa ilimbidi kujitokeza ili kumpigiania babake ambaye ni mgonjwa wa saratani, kwani mswada huo ungeumuathiri pia kwa namna moja au nyingine.
“Nimekuwa nikishiriki maandamano haya kutoka siku ya kwanza, na nitajitokeza bado kushiriki kwa sababu baba yangu ni mgonjwa wa saratani, na wagonjwa wa saratani 3 hufa kila baada ya saa 3, na bado sasa hivi serikali inataka kutuongezea ushuru licha ya kwamba tunahangaika kulipia matibabu ya saratani, haiwezekani,” Matubia alisema.
Maandamano hayo ambayo yalikuwa ya kihistoria kwa kuingia katika majengo ya bunge yalimshangaza na kumtikisa rais Ruto kiasi kwamba siku moja baadae aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kukiri kwamba amekubali kuutupilia mbali mswada huo.