Mwanasosholaiti maarufu wa Kenya anayeishi nchini Dubai, Huddah Monroe, ameweka wazi kuwa si rahisi kwa wanaume kupata nambari yake ya simu.
Katika chapisho kwenye akaunti yake ya Instagram, mrembo huyo alifichua kwamba mtu lazima alipe angalau $3000 (Sh387,240) ili kupata nambari yake.
Huddah alitoa tangazo hilo chini ya video ya mwanamume aliyekiri kulipia kodi ya nyumba ya mwanamke ili kupata nambari yake ya simu. Katika ujumbe wake, aliagiza kwamba mtu anayehitaji nambari yake anahitaji kutuma pesa kwa sarafu ya bitcoins.
“Watu wanaosema kumlipia kodi ni jambo la kutatanisha, kupata nambari yangu ya simu inagharimu $3000. Tuma bitcoin haraka iwezekanavyo,” Huddah alisema kwenye video hiyo aliyoichapisha siku ya Jumatano.
Mwanasosholaiti huyo alidokeza kuwa si ajabu kwa wanaume kumtumia bitcoins kabla ya kupata nambari yake ya simu.
"Nimezoea wanaume kuuliza anwani ya btc kabla ya nambari ya simu," alisema.
Huddah, ambaye ni miongoni mwa wanasosholaiti maarufu zaidi wa Kenya, anaishi Dubai kwa sasa. Sio mengi yanayojulikana kuhusu mahusiano yake ya sasa wala sio wazi ikiwa anachumbiana na mwanaume yoyote.
Miezi kadhaa iliyopita, mwanadada huyo mrembo aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram ambapo alijibu baadhi ya maswali kuhusu maisha yake.
Moja ya maswali muhimu aliyoulizwa ni kwa nini bado hajapata mwanaume wa kumuoa rasmi licha ya urembo wake wa kuvutia.
“Mbona mpaka leo hujaoleka wakati wewe ni mrembo?,” mtumizi wa Instagram alimuuliza.
Katika majibu yake, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 31 alidokeza kuwa ndoa si ndoto yake akiashiria kuwa si jambo rahisi.
Wakati huohuo, alifichua kwamba hata ikiwa angechukua hatua ya kuingia kwenye ndoa, angeiweka faragha mbali na macho ya umma.
“Umeshawahi kujiuliza si ndoto ya kila mtu. Ndoa sio matembezi kwenye bustani (si rahisi). Ni ngumu kuliko unavyofikiria. Na kama ningeolewa usingejua. Hilo litakuwa la faragha milele,” Huddah Monroe alisema.
Mrembo huyo wa Kenya ambaye wakati mwingine anaishi Dubai kwa muda mrefu amekuwa msiri kuhusu mahusiano yake.
Hapo awali, Huddah alikuwa amedaiwa kutoka kimapenzi na mwimbaji wa Tanzania Juma Jux baada ya wawili hao kuonekana wakiwa pamoja mara kadhaa. Wawili hao hata hivyo baadaye walijitokeza kuweka wazi kuwa hakuna mahaba kati yao na kudai kwamba uhusiano wao ni wa kirafiki na kibiashara tu.
Katika kipindi cha Maswali na Majibu cha mwaka jana, mwanasosholaiti huyo alifichua kuwa 'mahusiano' yake na Jux yalikuwa ni mradi tu ambao walikuwa nao pamoja na tayari ulikuwa umeisha kufikia mwezi huo.
"Kama Raila, Ulikuwa tuu mradi. Na uliisha," Huddah alisema kwenye Instagram.