Mastaa wa Bongofleva, Harmonize wa Konde Music Worldwide na Diamond Platnumz wa WCB wameonekana kurudi katika kuzozana hadharani.
Siku ya Alhamisi, wasanii hao ambao mara nyingi huchukuliwa kuwa wanamuziki wakubwa zaidi nchini Tanzania walichapisha machapisho kwenye mtandao wa Instagram ambayo yalionekana kuwa mashambulizi yasiyo ya moja kwa moja dhidi ya kila mmoja wao.
Diamond Platnumz ndiye aliyeanza mashambulizi hayo kwa kuchapisha screenshot ya chati ikimuonyesha kama mwanamuziki wa Tanzania ambaye alitazamwa zaidi kwenye YouTube mwezi wa Juni.
“Simba na wanawe,” Diamond aliandika chini ya chati hiyo aliyoichapisha.
Katika chati hiyo, bosi huyo wa WCB alitazamwa na watazamaji 33.7m mnamo mwezi Juni, Rayvanny alikuwa na watazamaji 23.1m, Zuchu alishika nafasi ya tatu akiwa na watazamaji milioni 13.7, Mbosso alikuwa na views milioni 11.6 huku Harmonize akishika nafasi ya 5 akiwa na watazamaji milioni 11.
Huku akionekana kumjibu bosi huyo wake wa zamani WCB, Konde Boy alichapisha chati mbili zilizomuonyesha akiongoza.
“Hawawezi kupost hii!! Ni wakati wa Ibraah hata hivyo,” Harmonize aliandika kwenye chati ya wasanii bora katika wiki inayoanza Juni 21-Juni 27, 2024.
Bosi huyo wa Kondegang aliongoza orodha hiyo, huku Diamond Platnumz akifuatiwa na Rayvanny na Zuchu wakishika nafasi ya tatu na ya nne.
Chati ya pili aliyochapisha ilionyesha orodha ya video bora za muziki katika siku moja Juni 29, 2024 ambapo wimbo wake na Rayvanny ‘Sensema’ ulioongoza siku hiyo.
"Uko wapi baba," aliandika.
Wimbo ‘Siji’ wa Zuchu, Binadamu wa Kontawa na Disconnect wa Harmonize zilifuata kwa njia mfululizo kulingana na chati.