Zari azungumzia uhusiano wa karibu na wanawe wakubwa, aonyesha picha zao wakiwa watoto

Zari alichukua nafasi kutambua jukumu lake katika maisha ya mbegu za kwanza za tumbo lake.

Muhtasari

•Zari Hassan alichapisha picha za kumbukumbu zake na vijana hao watatu wa kiume tangu walipokuwa wadogo.

•Kwa sasa ameolewa na Shakib Cham Lutaaya na tayari wawili hao wamedokeza kuhusu kupata watoto pamoja.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasosholaiti mashuhuri wa Uganda Zari Hassan amewasherehekea wanawe watatu wakubwa kwa njia maalum sana.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumamosi asubuhi, mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 43 alichapisha picha za kumbukumbu zake na vijana hao watatu wa kiume tangu walipokuwa wadogo.

Zari alitumia fursa hiyo kutambua jukumu lake katika maisha ya mbegu za kwanza za tumbo lake na kufichua kwamba daima atakuwepo daima  kwa ajili.

"Kazi yangu kama mama haitaisha. Kwa sasa, nitakuwa kila kitu kwenu, lakini mtakuwa kila kitu kwangu kila wakati. Jana, wavulana wangu wadogo, leo, marafiki zangu and daima wanangu,” Zari aliandika chini ya picha alizochapisha.

Mwanasosholaiti Zari Hassan alizaa wanawe watatu wakubwa, Pinto Tlale, Raphael Ssemwanga na Quincy Tlale, miaka mingi iliyopita alipokuwa kwenye ndoa yake ya kwanza na marehemu mfanyabiashara wa Uganda Ivan Ssemwanga.

Mfanyabiashara huyo mrembo ambaye kwa sasa anaishi nchini Afrika Kusini pia ana watoto wengine wawili, wa kiume na wa kike, aliowazaa alipokuwa kwenye ndoa na mwanamuziki wa Tanzania Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz.

Kwa sasa ameolewa na mfanyabiashara kutoka Uganda, Shakib Cham Lutaaya na tayari wawili hao wamedokeza kuhusu kupata watoto pamoja.

Shakib ameonekana kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na watoto wadogo wa Zari kuliko vijana hao wakubwa.

Mapema mwaka huu, Shakib alichapisha video nzuri zake na watoto wawili wadogo wa mkewe Zari wakifurahia muda pamoja kwenye ukumbi wa mazoezi. Alionekana akiwasaidia watoto hao wa Diamond kufanya mazoezi kwa kutumia vifaa tofauti kwenye gym moja nchini Afrika Kusini ambako wanaishi.

Katika video za kwanza, mfanyibiashara huyo wa Uganda alionekana akiwainua Tiffah na Nillan hadi kufikia nguzo ambayo ilikuwa juu sana na kuwasaidia kufanya mazoezi. Baadae alionekana akiwatazama wawili hao walipokuwa wakivuta kamba nzito ya mazoezi kabla ya kuwapa mafunzo ya ndondi.

"Wakati wa kusonga," Shakib alisema chini ya video iliyomuonyesha akiwafundisha watoto hao wawili mitindo ya ndondi.

Hapo awali, Zari alikuwa ameshiriki video nzuri ya mume wake Shakib akikaribishwa nyumbani na binti yake Tiffah  kwa njia ya kupendeza sana.

Katika video hiyo ambayo Zari alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Tiffah ambaye ni mtoto wa kwanza wa mwanasosholaiti huyo na Diamond Platnumz alionekana akimkimbilia Shakib alipokuwa akishuka kwenye gari lake.  

Punde baada ya malkia huyo wa miaka minane kufika pale alipokuwa Shakib, babake huyo wa kambo alimkumbatia vizuri na kumuinua kwa mikono miwili. Wawili hao kisha walionekana kuwa na mazungumzo mafupi nje ya gari.

Zari alionekana kufurahishwa sana na uhusiano mzuri ulioonyeshwa kati ya mumewe huyo mwenye umri wa miaka 32 na bintiye. Aliambatanisha video yake na wimbo “I love you baby” wa Emilee.