Harmonize amefunguka kwamba hana tatizo lolote la kufanya kolabo na Alikiba, licha ya wengi kufikiria kwamba wawili hao hawaelewani kutokana na ushindani wao kimuziki.
Aidha, msanii huyo amefichua kwamba moja kati ya nyimbo zake akianza ulikuwa umepata msukumo kutoka kwa nyimbo za Alikiba.
Alisema kwamba anaamini katika safari yake ya muziki, asingekuwa Harmonize wa sasa pasi na mchango wa watu hivyo kusema hatochagua msanii wa kufanya kolabo naye ikiwa mashabiki wake watataka ifanyike.
Kwa maneno yake, Harmonize alisem;
“Mimi wakati linakuja suala la muziki kila kitu naweka pembeni nawaheshimu sana mashabiki, nauheshimu sana muziki, kwa hiyo demand ya mashabiki ambao ndio wamenifanya nikawa hivi, wakisema tunahitaji wimbo ufanye na msanii fulani, mbona nikatae?”
“Msanii yeyote mimi sina noma, niko hivyo kwa sababu naamini kila mwanamuziki ana mchango wake ambao umenifanya mimi nikawa hapa. Ukisikiliza wimbo wangu wa zamani kidogo unaitwa ‘Niambie’ ni inspired by wimbo wa Alikiba unaitwa ‘Nikiss’.”
Msanii huyo alizidi kueleza kilichomvutia kwa wimbo huo wa Alikiba kiasi kwamba akaamua kutunga wimbo wenye maudhui sawia.
“Nilipata inspiration nikaona ni topic ambayo kila mtu anaweza akapenda kwa sababu baadhi yetu ambao tumetoka kwenye familia za kimasikini tunapenda sana kulalamika kwa sababu maisha yetu sio mazuri, yaani hata ukitelekezwa kwenye mapenzi hisia za kwanza zinakutuma kufikiria umeachwa kisa huna pesa, hivyo nikapenda ule wimbo. Na ndio nasema kila mwanamuziki ana mchango wake kwenye maisha yangu ya muziki,” alisema.