Msanii Harmonize kwa mara ya kwanza amejibu ni kwa nini hajawahi fanya kolabo nyingine na rafiki yake mkubwa kutoka Nigeria Burna Boy licha ya kudai kuwa mtu wake wa karibu tangu walipofanikisha kolabo ya kwanza na ya pekee ya ‘Kainame’ mwaka 2019.
Bosi huyo wa Konde Gang amefichua kwamba ni kweli kwa sasa hawana ukaribu sana na Burna Boy kwa kile alikitaja kuwa msanii huyo wa Nigeria ameshakuwa mtu mkubwa na tajiri hivyo pengine amebadilisha marafiki, lakini akasema kuwa kutoongea kwao sana haimanishi kwamba wameshakuwa maadui.
“Sisemi uongo, Burna Boy ni mtu wangu lakini si mtu wangu wa karibu saana sasa hivu, yule kawa tajiri sana. Mimi na yeye tunafahamiana, tumekuwa marafiki, tumeshiriki moments nzuri pamoja, tumesharekodi ngoma ambazo zimetoka, zingine ambazo hazijatoka...”
“Siwezi nikakaa hapa nikasema ti unajua Burna Boy tunaongea kila siku, aah hapana. Nitakuwa nadanganya, kwa sababu kama tungekuwa tunaongea kila siku jamani shoo zake zile za kujaza viwanja si ningekuwa hata mimi ningeenda nikasema ‘sold out’. Hatuzungumzi san asana lakini hiyo haibadilishi kwamba si mtu wangu, si rafiki yangu,” alisema.
Pia alisema muda mwafaka ukifika watakutana na wakiona kuna haja ya kutoa kibao cha pamoja hakuna kitakachozuia.
“Tumekutana kama wanamuziki, sisi ni marafiki tukikutana tutasalimiana na tuna mpango wa kutoa hizo nyimbo, zisipotoka pia hakuna tatizo.”