Mfanyibiashara Jimal Rohosafi amemtaka rais William Ruto kumuangazia jicho wakati atakapoteua baraza lake jipya la mawaziri.
Hii ni baada ya rais Ruto kutangaza kuvunjiliwa mbali kwa baraza la mawaziri Alhamisi alasiri, baada ya malalamishi mengi kutoka kwa vijana kuhusu utendakazi wa serikali yake.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jimal alichapisha ujumbe akijipigia debe na kusema kwamba safari hii ni ama yeye au mwenzake, Khalif Kairo, sharti mmoja wao awe waziri.
Jimal alisema asipofaulu basi mwenzake, mfanyibiashara wa kuuza magari, Khalif Kairo, lazima awe waziri katika wizara ya barabara, miundombinu na uchukuzi.
“Khalif Kairo, ni au mimi ama wewe, lazima mmoja wetu awe waziri wa barabara na uchukuzi kabla Baba [Raila Odinga] aseme anataka nafasi 6 za mawaziri,” Jimal alisema.
Aidha, mpenzi huyo wa zamani wa mwanasosholaiti Amber Ray alisisitiza kwamba vijana wa Gen Z pia wanastahili kupata angalau nafasi 10 za mawaziri katika serikali ya Ruto, ikizingatiwa juhudi zao kubwa ambazo zimezaa matunda kwa kuishinikiza serikali kupitia maandamano wiki mbili zilizopita.
“Sisi tunataka wizara 10 (Gen Z). Tafadhali chapisha kwenye kurasa zenu majina ya vijana wa Gen Z ambao mngewataka kuwa mawaziri,” aiongeza.
Baada ya kulitupilia mbali baraza lake la mawaziri, Ruto alisema atachukua muda wake wa kufanya mashauriano na makundi mbalimbali ya watu ili kuchagua mawaziri wapya watakaomsaidia kuendesha serikali.