Msanii Stevo Simple Boy ametoa wito kwa rais William Ruto kumteua kuziba pengo lililoachwa kwenye wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na turathi za Kitaifa.
Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram, rapa huyo anayejitambua kama rais wa wanyonge alisema kwamba yuko radhi kuchukua nafasi ya aliyekuwa waziri katika wizara hiyo, Aisha Jumwa.
Simple Boy alisema kinachompa msukumo wa kuomba kuteuliwa katika wizara hiyo ni kwamba anataka kuwatetea wasanii wenzake.
“Ningependa kufikisha ujumbe kwa rais William Ruto, ulifuta baraza lote la mawaziri, mimi kama rais wa Wanyonge, unipatie hicho cheo ambacho ulikuwa umempa Aisha Jumwa. Kiti cha Sanaa, nipatie nitetee wasanii wenzangu,” Simple Boy alisema huku akimteg rais Ruto.
Rais Ruto alitangaza kulivunjilia mbali baraza lake la mawaziri mnamo Julai 11 akiwemo mwanasheria mkuu wa serikali lakini akasalia na waziri mwenye mamlaka makuu ambaye pia ndiye waziri wa masuala ya kigeni, Musalia Mudavadi.
Tangu wakati huo, watu mbalimbali wamekuwa wakijitokeza na kuonyesha azma ya kutaka kufanya kazi kwenye baraza jipya la mawaziri litakaloteuliwa siku si nyingi kutoka sasa.
Mfanyibiashara Jimal Rohosafi mwishoni mwa juma lililopita alionesha nia ya kutaka kuteuliwa kama waziri wa barabara na uchukuzi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Kipchumba Murkomen.
Katika ujumbe wake kwenye Instagram, Jimal Rohosafi alisema kwamba ni sharti ima yeye au mwenzake anayejishughulisha na biashara ya kuuza magari, Khalif Kairo, mmoja wao sharti awe waziri wa barabara na uchukuzi.
Sasa macho yote yanaelekezwa kwa rais Ruto ambaye anatarajiwa kuliteua baraza jipya la mawaziri na tayari ameliomba kanisa na taifa kwa ujumla kumuombea anapofanya maamuzi ya uteuzi wa mawaziri wapya.