Nandy na Billnass wamesherehekea miaka miwili tangu kufunga ndoa kwa mtindo wa kipekee.
Kupitia Instagram, Nandy alichapisha video ya zawadi aliyomtunuku mumewe, Billnass kama kumbukumbu ya miaka miwili kwenye ndoa.
Nandy alimchukua mbuzi wa rangi nyeupe na kumfungia ndani ya gari la kifahari la Billnass katika kiti cha dereva.
Kisha alimuita mumewe na kumtaka kufungua gari lake na kwa mshangao wa Billnass, alikutana na mnyama mbuzi kafungwa kwenye usukani.
Nandy alieleza kwamba zawadi ya mnyama mbuzi ni ishara ya kipekee kuashiria heshima katika kabila la Wachaga, na hivyo kumtaka Billnass kujihisi kuheshimika kaitka ndoa yao.
“Mume wangu jukumu langu ni kuhakikisha huna stress, una furaha, amani, na unakula vizuri! Pokea zawadi yangu hii ! MBUZI kwa wachaga ni kitu cha heshima sana kama zawadi. Basi na me nikuahidi afya bora na mapenzi tele,” Nandy aliandika.
Kwa upande wake, Billnass alimshukuru mkewe kwa zawadi hiyo ya kumbukumbu ya miaka miwili kwenye ndoa ambapo wamebarikiwa na mtoto wa kike, Kenaya.
“Ahsante Kwa Zawadi Mke Wangu ❤️…leo ni Mbuzi na bia Tu !! Au Nimfuge Inaweza kuwa Biashara,” Billnass alitania.
Wawili hao walifunga ndoa mwaka wa 2022, ndoa ambayo hata hivyo ilipokea kejeli kutokana na dhana kwamba walifanya harusi wakati ambapo tayari Nandy alikuwa mjamzito, jambo ambalo baadhi walihisi si sahihi kwa kanisa kuifungisha harusi hiyo.