Huku rais William Ruto akitarajiwa kutoa tangazo muhimu majira ya saa kumi alasiri atakapokuwa akilihutubia taifa, kumekuwa na tetesi kwamba huenda akatangaza baraza lake jipya la mawaziri.
Wakati uo huo, Watu katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakikisa ni nani huenda atateuliwa katika wizara ipi, baada ya rais Ruto kushinikizwa na vijana wa Gen Z hadi kulivunja baraza lake la mawaziri.
Aliyekuwa seneta maalum Millicent Omaga amejitokeza na kudai kwamba amesikia amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii huku akiibua hoja kwamba huenda yuko miongoni mwa majina yatakayotajwa na rais atakapotangaza baraza lake la mawaziri.
Omanga katika ukurasa wake kwenye jukwaa la X amewauliza wafuasi wake kumpa maoni wapo atakataa au atakubali endapo rais Ruto atamteua katika baraza lake la mawaziri.
“Nimekuwa nikivuma huko nje. Kutoka kinywani mwako hadi masikio ya Mungu. Mnaonaje? Nikipewa nianguke nayo ama?” Omanga aliuliza.
Itakumbukwa Omanga alikuwa miongoni mwa majina 50 yaliyopendekezwa na rais Ruto kuchukua nafasi za wasaidizi wa mawaziri, CAS, nyadhifa ambazo zilitupiliwa mbali na mahakama.
Omanga alikuwa ameteuliwa kama CAS katika wizara ya usalama wa ndani.