Kennedy Rapudo na mkewe Amber Ray wamezungumzia uzoefu wao katiak kumlea mwanao wa pamoja, Africanah Rapudo.
Wawili hao ambao walikuwa miongoni mwa hadhira katika urekodiwa kwa shoo ya uchekeshaji ya Churchill katika mgahawa wa Carnivore jijini Nairobi, walizungumza na waandishi wa habari za burudani, walionyesha furaha yao kushiriki safari ya malezi ya mwanao.
Rapudo alisema kwa utani kwamba binti yake ana makuzi mazuri lakini akatania kwamba tabia ya kichwa ngumu ndio tu amerithi kutoka kwa mama yake, ambaye ni Amber Ray.
“Africanah ana unajua zile tabia nzuri kuna mahali zimetoka lakini hicho kichwa ngumu kidogo ni ya mamake, lakini yote kwa yote yeye ni kichwa ngumu kwa njia nzuri. Mimi muda wote huwa napenda watu ambao wanajua jinsi ya kuelezea wanachofikiria, napenda tabia shupavu zilizojitegemea na hicho ndicho kitu ambacho napenda kuhusu binti yetu na huwa namuona sana mama yake ndani yake,” Rapudo alisema.
Hata hivyo, Amber Ray alikanusha kuwa kichwa ngumu akisema kuwa Rapudo ndiye kichwa ngumu zaidi ikizingatiwa kwamba anatoka katika jamii ya Dholuo.
“Wewe mpenzi wangu ndiye kichwa ngumu, ni vile tu kwamba watu hawakujui sana hapa nje, wewe kama Mluo,” Ray alisema.
Wawili hao walisherehekea siku ya kuzaliwa ya Africanah ambaye alifikisha umri wa mwaka mmoja miezi kadhaa iliyopita.
Amber Ray ambaye hivi majuzi alionekana akimtafutia shule mtoto huyo wa mwaka mmoja alieleza sababu ya kutaka kumpeleka shule katika umri mdogo hivyo.
“Najua ni mdogo lakini msichokifahamu ni kwamba yule binti ni mwenye akili nyingi. Ukipata nafasi ya kuketi na Africanah hapa huwezi hata fikiria kwamba ana umri wa mwaka mmoja na miezi 3. Unaweza dhani amefika umri wa zaidi ya miaka 2 ukisikia vile vitu anafanya, anasikia… nahisi kwamba kwetu sisi tukikaa naye nyumbani itakuwa kama tunamshusha chini,” Ray alisema.