Mwanasosholaiti Amber Ray amezungumzia uwezekano wake kuingia kwenye siasa katika uchaguzi mkuu ujao, 2027.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kurekodiwa kwa shoo ya uchekeshaji ya Churchill katika mgahawa wa Carnivore mwishoni mwa juma, Ray alisema kwamba huo wakati ukifika na Mungu aizungumzie nafsi yake, bila shaka atajitosa siasani.
Hata hivyo, mama huyo wa watoto wawili alisema kwa sasa hayuko tayari kuingia kwenye siasa, hata kama rais Ruto atampendekeza kuhudumu katka baraza lake la mawaziri, atakataa uteuzi huo.
“Sasa hivi tuseme rais Ruto ameniteua nafasi ya CS, hapana, siwezi kubali, nitakataa kwa sababu huu ni wadhifa muhimu sana kwa mtu yeyote kushikilia. Kwangu mimi, nitachukua muda kuzama zaidi kwa kile watu wanahitaji ili niweze kuwawajibikia, unaelewa. Kwa sasa nahisi kama siko tayari kabisa hivyo siwezi kubali,” Ray alisema.
“Kwa upande wagu muda wote mimi huwa mtu wa kufuata maono kutoka Mbinguni, na huwa napiga hatua kwa wakati hivyo kama muda huo utafika na nijihisi kwamba niko tayari kwa hili, naweza fanya hili, mbona nisijaribu?” alisema.
Kwa upande wake, mumewe Kennedy Rapudo alimuunga mkono mpenziwe akisema kwamba ako na uhakika kama Amber atajitosa kwenye siasa na kuchaguliwa, atafanya mambo makubwa na kubadilisha maisha ya wengi.
“Yeye kuingia katika siasa, mbona isiwezekane? Niko na uhakika yeye kuingia katika siasa atafanya mambo makubwa na kubadilisha maisha ya wengi, atabadilisha maisha ya vijana na pia ataweza kuzungumzia wanawake, hivyo nina uhakika yeye ana uwezo zaidi.”
“Na muda wote mimi humuambia wakati wowote ako tayari kuanza kupiga kampeni aniambie na nitahakikisha kila kitu kiko tayari kwa ajili ya hilo. Hivyo, Amber muda wote ako na uungwaji mkono wangu, na familia pamoja na marafiki zetu,” Rapudo aliongeza.