Miracle Baby, msanii wa zamani wa Gengetone na Mugithi ambaye sasa amegeukia injili na hata kutangaza kuwa mchungaji ameonesha furaha yake baada ya wimbo wake wa kwanza wa injili kufikisha watazamaji milioni moja kwenye mtandao wa YouTube.
Kupitia kurasa zake katika mitandao ya kijamii, Peter Miracle Baby aliwashukuru mashabiki wake kwa kumpokea kwa njia nzuri katika mkondo wake mpya wa kujikita katika injili.
“Aki asanteni saana kwa kutufikisha 1millon views ,sasa naona injili ya bwana ikisonga,” Miracle Baby alisema.
Miracle Baby alishirikiana na mpenzi wake, Carol Katrue kutoa wimbo huo kwa jina Ndi Mwiria, miezi miwili iliyopita baada ya kutoka hospitalini.
Itakumbukwa msanii huyo alitumikia maisha yake mengi katika nusu ya mwaka huu akiwa hospitalini baada ya kupatwa na matatizo ya kujiradidi kwenye utumbo wake.
Miracle Baby alilazwa hospitalini kutoka katikati ya mwezi Januari hadi karibia mwezi Aprili ambapo alifanyiwa upasuaji zaidi ya mara tatu kutibu tatizo hilo.
Baada ya kutoka hospitalini, alitangaza bila kushrutishwa kwamba ameamua kumtumikia Mungu kwani yeye ndiye aliyeinusuru nafsi yake kutoka kwa ugonjwa huo.
“Nilisema nataka kuwa pasta na kuhubiri, unanielewa. Lakini kuhubiri kuko katika njia nyingi, mtu unaweza kuhubiri kupitia nyimbo, kwa sababu mtu kama mimi kwa sasa sina kanisa, wala sina eneo la kuweka kanisa,” Miracle Baby alisema.
Msanii huyo aidha alionesha Imani yake kuu kwamba Mungu atamfungulia njia na milango kupata eneo la kuanzisha kanisa, akionesha matumaini makubwa katika kufanikiwa katika mkondo huo mpya.
“Najua Mungu akitaka, atanipa eneo la kuweka kanisa na litakua, nikishapata eneo la kuweka kanisa, najua waumini watakuja kwa kweli. Kwa hiyo, yangu nimeianza kupitia muziki,” Miracle Baby alisema