logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Naanza safari ya kuwa single!" Size 8 atangaza kuachana na DJ Mo baada ya miaka 11

Katika taarifa fupi siku ya Alhamisi, m

image
na Samuel Maina

Burudani01 August 2024 - 11:23

Muhtasari


  • •Katika taarifa fupi siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto wawili alitangaza kwamba sasa anaanza safari ya kuwa bila mume.
  • •Size 8 amekuwa kwenye ndoa na mcheza santuri DJ Mo kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita na wana watoto wawili pamoja.

 Mchungaji na Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili nchini Kenya, Linet Munyali almaarufu Size 8, ametangaza kuvunjika kwa ndoa yake ya miaka kumi na moja.

Katika taarifa fupi siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto wawili alitangaza kwamba sasa anaanza safari ya kuwa bila mume.

Size 8 amekuwa kwenye ndoa na mcheza santuri Samuel Muraya almaarufu DJ Mo kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita na wana watoto wawili pamoja.

"Wakati mwingine ndoa hufanya kazi kwa neema ya Mungu, na wakati mwingine haifanyi kazi, lakini yote kwa yote Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi," Size 8 alisema kupitia Instagram.

Aliongeza, "Nimeolewa kwa miaka 11 na sasa ninaanza safari ya kuwa mseja. Lakini Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi, nakuabudu wewe Yaweh!"

Hata hivyo, mwanamuziki huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu hali ya ndoa yake au sababu iliyosababisha yeye kutengana na mzazi mwenzake.

Mapema mwaka huu, Size 8 alifichua kwamba aliwahi kutaka kugura ndoa yake na DJ Mo na hata akatafuta usaidizi wa wakili wa talaka.

Wakati akizungumza katika kipindi cha uhalisia kilichopeperushwa kwenye runinga ya TV 47, mama huyo wa watoto wawili alifichua kwamba alikuwa amepoteza matumaini katika ndoa yake kiasi cha kutaka kuivunja.

“Kilichofanyika, ilifika mahali nikawa sina matumaini, nikawa nimefika hatua ya kutorudi nyuma. Nadhani msongo wa mawazo pia ulianza. Kwa hivyo sikuwa nikifikiria sawa na sikuwa nikiona njia ya kutoka. Ndiyo maana niliamua kumwita wakili wa talaka,” Size 8 alisimulia.

Mwimbaji huyo alifichua kuwa baada ya kumweleza mwanasheria wa talaka kuhusu nia yake ya kuvunja ndoa yake, hata alimwelekeza aanze kutayarisha karatasi rasmi za hatua hiyo. Alisema kuwa alitaka kutenganishwa na mcheza santuri huyo na kuruhusiwa kwenda na watoto wao wawili.

Talaka hiyo hata hivyo haikuendelea baada ya mama huyo wa watoto wawili kuzungumza na mamake DJ Mo na pia kuhudhuria likizo ya mafunzo ambayoilimfanya apate hamu ya kuipa ndoa hiyo nafasi nyingine.

“Tuko karibu sana na mama yake. Aliniambia nimekasirika nisifanye mambo kwa haraka. Kisha mhubiri alikuwa ametaja likizo takriban wiki mbili kabla, ilikuwa imebaki mwezi hadi tarehe ya likizo. Nilisema, nitapatia ndoa yangu nafasi moja ya mwisho,” alisema.

Size 8 alisema baada ya kuhudhuria mafiunzo hayo, alikubali kutulia na kutazama iwapo mume wake naye angekuwa tayari kuifanyia kazi ndoa yao.

Akizungumzia kwa nini alitaka kuacha ndoa yake, mwimbaji huyo alisema kuna mambo mengi yalimfanya atake kumuacha mumewe.

"Nilipoenda huko, nilijifunza kweli. Mimi nilikuwa nataka kuacha Mo kwa sababu ya mingi. Yaani ni kama tulikuwa tunaenda njia pande," alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved