Siku chache baada ya msanii wa injili na mchungaji Size 8 kutangaza kuachana na mpenzi wake wa zaidi ya miaka 10, Dj Mo, seneta maalum Karen Nyamu ametilia kwenye mizani sakata hilo.
Nyamu kupitia Instagram yake alichapisha ujumbe wa kuwaomba wawili hao kusuluhisha tofauti zao na kurudi katika familia moja yenye furaha akisema kwamba kuachana kwa kweli aghalabu hakutangazwi mitandaoni.
Nyamu alisema kwamba kwa itikadi ya Size 8 kutangaza hadharani kwamba wameachana, huenda hiyo ni dhana tu bali kiuhalisia huenda wako pamoja ila wanapitia changamoto za kumfanya kuhisi kukata tamaa.
“Kuachana kwa kweli huwa hakuna tangazo. Wakati unaona tangazo kwenye mitandao ya kijamii hivyo jua tu kwamba wachumba hao wanapitia wakati mgumu kwa wakati huo. Tunawatakia Size 8 na Dj Mo mazuri katika ndoa yao. Tafadhali msichoke, hakuna mtu alisema itakuwa rahisi,” Seneta Nyamu alisema.
Katika taarifa fupi siku ya Alhamisi, Size 8, mama wa watoto wawili alitangaza kwamba sasa anaanza safari ya kuwa bila mume.
Size 8 amekuwa kwenye ndoa na mcheza santuri Samuel Muraya almaarufu DJ Mo kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita na wana watoto wawili pamoja.
"Wakati mwingine ndoa hufanya kazi kwa neema ya Mungu, na wakati mwingine haifanyi kazi, lakini yote kwa yote Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi," Size 8 alisema kupitia Instagram.
Aliongeza, "Nimeolewa kwa miaka 11 na sasa ninaanza safari ya kuwa mseja. Lakini Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi, nakuabudu wewe Yaweh!"