Kizaazaa kilizuka katika kanisa moja la Mwea, kaunti ya Kirinyaga, baada ya mwanamke aliyedai kuwa mke wa kasisi katika kanisa hilo kukatiza harusi ambayo mumewe waliyeachana naye alitazamiwa kutembea na mwanamke mwingine.
Nipango kabambe ilikuwa imeandaliwa kaitka kanisa hilo ambao mchungaji huyo alikuwa afunge pingu za maisha na mpenzi mpya mara ghafla mkewe akaingia kanisani kwa fujo akiandamana na wanao 5 hafla ya kufunga harusi ikiendelea.
Akiwa na watoto wake watano, Rose alisimamisha sherehe katika azma yake ya kumzuia Mchungaji Chomba asitembee kwenye njia hiyo.
Kulingana na mke huyo aliyetambulika kwa jina Rose, ndoa yao ilifanyika mwaka 2013 lakini akasisitiza kwamba bado iko halali kwani hawakutalikiana kirasmi.
“Tulienda kanisani kufungisha ndoa yetu kulingana na kanuni za kisheria na ilikubaliwa na parokia ya Kerugoya, kwa hivyo ninashangaa jinsi anavyooa mke mwingine bila sisi kujua,” alieleza.
Mzozo ulianza wakati timu ya usalama ya kanisa ilipinga majaribio ya Rose ya kusimamisha harusi huku sehemu ya waumini na wageni wakihoji kuhusu wakati wake.
“Tunashangaa kwa nini wanakuja wakati huu licha ya muda wote wa kuweka pingamizi wakati wa maandalizi,” alibainisha mshiriki mmoja wa kanisa hilo ambaye hakufurahishwa na mabadiliko hayo.
Rose aliyekasirika alidai kuwa mumewe alimtelekeza na watoto watano na kwenda kuishi kwa mke mpya ambaye alitarajia kufunga naye harusi.
Majaribio ya awali ya kusuluhisha suala hilo yaliambulia patupu, hivyo kumuacha bila chaguo ila kujitokeza katika siku kuu ya mume wake aliyeachana naye.
Alizidi kumshutumu kwa kupanga kuuza ardhi ya familia baada ya kufanikiwa kutelekeza familia.
"Mama yangu alikuwa akihangaika kutupeleka shule, sasa tunashuku anataka kuoa mwanamke mwingine ili wauze ardhi yetu na kutuacha bila chochote," alibainisha mmoja wa watoto hao.
Polisi kutoka kituo cha polisi cha Wanguru waliitwa ili kudhibiti hali hiyo.