Mfanyibiashara Murugi Munyi ametangaza kufunga biashara yake ya duka la nguo baada ya kuhudumu kwa miaka miwili.
Akitoa tangazo hilo kupitia Instagram Live siku moja iliyopita, Munyi alisema kwamba ni uamuzi mgumu ambao anauchukua lakini ilibidi kwani biashara hiyo haijakuwa ikileta faida katika siku za hivi karibuni.
“Imekuwa miaka miwili tangu nifungue Wild by Murugi, stoo yangu ambapo tunauza nguo, vito na begin a vitu vingine, na sasa kiwa ni baada ya kusherehekea kumaliza miaka miwili, sherehe ambayo tulifanya wiki jana, nimefanya uamuzi wa kufunga biashara hiyo na hivyo mwisho wa mwezi Agosti utakuwa hitimisho la Wild by Murugi kama mnavyoijua,” Munyi alitangaza.
Mjasiriamali huyo alieleza sababu za kufanya uamuzi huo akisema ni matumaini yake kwamba maamuzi yake hayajamshtua mtu yeyote.
“Kuna vitu vingi ambavyo vimenipelekea kufanya uamuzi huu. La msingi ni kwamba kibinafsi sijihisi kwamba niko katika sehemu niliyokuwa miaka miwili iliyopita nilipofungua hii biashara. Miaka miwili iliyopita nilikuwa Murugi Munyi tofauti, nilikuwa mjasiriamali tofauti, nilikuwa mke na mama tofauti, na mengi yametokea kati ya wakati huo na sasa ambayo yamenipelekea kufanya uamuzi huu,” alifafanua.
Mama huyo alisema kwamba bidii na uchu wa kuchakarika na kutafuta pesa za ziada ambao alikuwa nao wakati anafungua biashara hiyo kwa sasa umepungua.
Munyi alisema kwamba uchu wake wa kuchakarikia pesa za ziada na kutumia vizuri muda wake wa ziada uliisha baada ya mume wake kuenda nchini UK na kumlazimu kuanza kushughulikia malezi ya wanao peke yake.
“Nilipofungua biashara, nilikuwa nimezama zaidi kaitka ulimwengu wa kuchakarika, nilikuwa najiuliza nini naweza fanya na muda wangu wa ziada, ni wapi naweza tengeneza pesa za ziada, na nafikiri hivyo sivyo niliyo sasa. Nafikiri hili lilitokana na baada ya Zak kuenda UK mwaka jana, na nikabaki nikiwatunza watoto peke yangu, iliniweka katika hali ya kujifikiria, ni nini haswa maisha yangu yanahusu?” alisema.