Afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya kusafirisha watalii ya Bonfire Adventures, Simon Kabu amefichua kwamba yeye alianza kupokea malipo yake kutoka kwa maudhui yake katika mtandao wa Facebook mwezi Aprili mwaka huu.
Kabu alifichua haya saa chache baada ya Meta, kampuni mama ya Facebook na Instagram kutangaza kwamba wamezindua kipengele cha kuwalipa Wakenya kutokana na maudhui yao kwenye mtandao huo mkubwa zaidi wa kijamii duniani.
Kabu alithibitisha kuanza kulipwa Aprili akifuatisha na picha ya ithibati ya malipo hayo ambapo alipokezwa dola 3.88 mwishoni mwa mwezi Mei.
“Je, umeanza kupata mapato kutoka kwa Facebook? Fikiria walianza kunilipa kutoka Aprili 2024? Nifuate,” Kabu aliandika kwenye Facebook yake.
Meta ilitangaza Jumanne kwamba watumizi wa mtandao wa Facebook nchini Kenya wataanza kulipwa kutokana na maudhui ambayo watachapisha video asilia kwa mfumo wa reels kwa lugha za Kiswahili na zingine.
Kenya imekuwa nchi ya nne barani Afrika kwa watu ambao wanalipwa na Facebook kwa maudhui yao.
Nchi zingine ambazo watumizi wa Facebook wanalipwa ni pamoja na Afrika Kusini, Misri na Nigeria.