Muigizaji wa Kenya Nyaboke Moraa ameendelea kumuomboleza binti yake Marie Blak Achieng, siku kadhaa baada ya msichana huyo wa miaka 19 kupoteza maisha yake.
Ibada ya kumkumbuka marehemu Marie ilifanyika katika kanisa la t CITAM, Embakasi siku ya Jumatano wakati Moraa alipokumbuka jinsi alivyojifungua mtoto huyo wake wa kwanza akiwa msichana mdogo sana.
Alisema kwamba alikuwa bado kijana mdogo wakati Marie alizaliwa na akabainisha kwamba walifanya kumbukumbu nyingi pamoja kabla ya kukutana na kifo chake mnamo Julai 28.
"Sijui jinsi ya kumuomboleza mtoto wangu, moyo wangu umevunjika. Moyo wangu umevunjika sana. Tulikuwa na kumbukumbu nzuri sana,” Moraa aliwaambia waombolezaji wenzake.
Aliongeza, “Moyo wangu umevunjika. sijui nitamuachilia aje mtoto wangu. Kuna wakati fulani maishani nilikuwa nikipitia mengi na alinikuta nimevunjika chumbani ananiambia ‘mum hukuwangi mtu mbaya, watu tu wako nawe ndio wabaya’.”
Muigizaji huyo mcheshi aliendelea kuzungumza kuhusu jinsi imekuwa vigumu sana kwake kukubali kuwa binti yake ameaga dunia.
“Marie alikuwa mtoto mzuri. Moyo wangu umevunjika *2. Sijui nitamwambiaje mtoto wangu aje apumzike kwa amani. Sina nguvu ya kumwambia mtoto wangu apumzike kwa amani. Bado siamini kuwa mtoto wangu amepumzika,” alisema Nyaboke kabla ya kuzidiwa na hisia.
Marrie Achieng, ambaye alikuwa mzaliwa wa kwanza wa Nyaboke Moraa alipoteza maisha katika hali isiyojulikana mnamo Jumapili, Julai 28.
Siku moja baada ya tukio hilo la kusikitisha, muigizaji huyo mahiri aliomboleza binti yake katika chapisho la kwanza la mtandao wa kijamii tangu kifo chake cha kusikitisha.
"Nitaanzia wapi?" Nyaboke Moraa alisema kupitia mtandao wa Facebook.
Pia alichapisha video ya kumbukumbu iliyomuonyesha akicheza dansi na marehemu binti yake na kuiambatanisha na emoji ya mapenzi.
Siku hiyo hiyo, mzazi mwenza wa Bi Moraa, mfanyabiashara Blak Aende pia aliomboleza kifo cha binti yao Marrie Achieng.
Blak Aende aliandika kumbukumbu fupi na ya kihisia kwa binti yake akisema kwamba Jumapili ilikuwa moja ya siku mbaya zaidi maishani mwake.
"Ni Siku ya giza. Siwezi kumhoji Mungu, ninamwachia kila kitu (Mungu)," Blakaende aliandika kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Baadaye aliweka chapisho lingine likimuonyesha akiwa ndani ya ndege akisafiri nyumbani na juu yake akaandika, "Safari ya ndege ngumu zaidi kuchukua," ikisindikizwa na emojis za moyo mweusi.