Mambo yanaonekana kuchemka haraka sana katika ndoa ya sosholaiti wa Uganda Zari Hassan na mfanyibiashara Shakib Cham Lutaaya.
Wawili hao walifunga ndoa rasmi mwaka jana lakini Shakib mara kadhaa ameibua wasiwasi kuhusu uhusiano wa karibu wa mkewe na mzazi mwenzake, Diamond Platnumz, jambo ambalo sasa Zari ameibua malalamishi makubwa kuhusu.
Akimzungumzia mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 32 kupitia kipindi cha moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii, Zari alimuonya kuhusu wasiwasi wake akisema kuwa mumewe haleti chochote mezani kufaa yeye kujieleza kila mara.
“Lazima niwe hapa kila siku nikijitetea kwako?. Jamani, unaleta nini mezani ili niwe hapa nje nikikuhakikishia? Unaleta nini mezani ili niendelee kuthibitisha msimamo wangu?,” Zari alimwambia mumewe kwa hasira.
Mama huyo wa watoto watano aliendelea kumhakikishia mumewe kwamba anampenda, lakini akamuonya kuhusu kutilia shaka uaminifu wake.
“Mimi siko kama wewe. Najiamini sana. Nami nilikuchagua wewe. Kwa kutojiamini kwako, unafikiria vinginevyo, sidhani kama niko wako, labda unapaswa kuchumbiana na watu ambao wako kwenye kiwango chako. Unaleta nini mezani, ili niwe hapa nje nikijitetea kwako,” alisema.
Zari alisisitiza kuwa hana uhusiano wowote wa kimapenzi na mzazi mwenzake Diamond, na akabainisha kuwa alimchagua Shakib badala yake.
Pia aliweka wazi kuwa kuna wanaume wengi wakiwemo matajiri na watu mashuhuri wanaomtaka lakini bado alimchagua Shakib.
"Nilimchagua mume wangu. Kuna watu wengi huko nje ambao wanataka kuwa na mimi. Na ninaposema mengi, hawa ni watu ambao hamjui. Kuna watu wengi ambao wanataka kuwa na mimi na nilichagua mume wangu,” alisema.
Aliongeza, "Na katikati ya haya, mume wangu bado yuko hapa akifikiria kuwa nataka kuwa na baba watoto wangu. Unafikiri baba watoto wangu ni mshindani wako? Labda unahitaji nikutumie meseji za wanaume, wagombea urais wanaonitumia meseji, basi ujue ni nani mshindani wako?”
Sosholaiti huyo mrembo alibainisha kuwa anajua mumewe anampenda na akaweka wazi kuwa yeye pia anampenda sana.