Msanii na mfanyibiashara Kevin Kioko maarufu kama Bahati ameshangaza mashabiki wake mtandaoni baada ya kukiri kuwa yeye ndiye humvisha mkewe nguo zote.
Bahati alifichua haya mwishoni mwa juma walipotokea na mkewe kwa ajili ya hafla ya chapa moja ya unga wa ugali ambayo wamekuwa mabalozi wa mauzo kwa muda mrefu.
Bahati na Diana Marua waliposhuka kutoka kwa gari lao la kifahari aina ya Range Rover la rangi ya samawati, waandishi wa habari za burudani waliwakaribisha na bila kusita wakasifia muonekano wao.
Hata hivyo, mmoja alivutiwa na jinsi Diana Marua alikuwa amevishwa nadhifu na kutaka kujua nani alifanya kazi hiyo ya kupendeza.
Kwa mshangao wa wengi, Bahati alikiri japo kwa utani kwamba ni kazi ya mikono yake kumvisha mkewe nguo zote, akisema kuwa hadi sidiria yeye humvisha.
“Kawaida ni mimi huwa namvisha, mnajua kufunga bra si rahisi,” Bahati alisema huku akicheka na kukwepa maswali mengine.
Wanandoa hao aghalabu huwa si wasiri kwa mambo ya chumbani katika ndoa yao, hulka ambayo mara nyingi imekuwa ikisutwa na baadhi ya watu mitandaoni huku mashabiki wao kindakindaki wakionekana kufurahia kufuata safari ya maisha yao ya ndoa.