Msanii Bahati amedai kwamba anatengeneza pesa nyingi kuliko baadhi ya wabunge nchini Kenya.
Aizungumza na waandishi wa habari za burudani katika kaunti ya Kirinyaga wikendi iliyopita wakati wa hafla ya chapa anayotangaza, Bahati alidokeza kwamba sababu yake ya kuingia kwenye siasa haikuwa na msukumo wa kupata pesa zaidi, kwani pesa anazozipata ni nyingi kuliko mbunge.
Msanii huyo alitania zaidi kwamba kuna wabunge wengi tu ambao kwa sasa hawamiliki gari la kifahari aina ya Range Rover kama lile alilomnunulia mkewe Diana Marua wakati wa kusherehekea miaka 7 ya ndoa yao.
“Bado nina uwezo wa kuwasaidia watu wa Mathare bila kuwa Mbunge wao. Ninataka kurudi huko na wakfu wangu niendelee kuwasaidia, si lazima tungoje tuchaguliwe. Kwa sababu ninatengeneza pesa nyingi kuliko mbunge. Kama mbunge analipwa 900k, hiyo si kitu kwangu?”
“Kuna wabunge wengi hata hawaendish lile Range Rover lenye nilinunulia mke wangu. Sikuwania juu ya pesa ni vile tu nilitaka kufanya athari chanya lakini bado naweza fanya hivyo hata bila kuwa MP. Lakini nikipewa nafasi nitafanya hata zaidi,” alisema.
Msanii huyo aliingia kwenye siasa na kujaribu bahati yake wakati wa uchaguzi wa 2022.
Aliwania wadhifa wa eneo bunge la Mathare kwa tikiti ya chama cha Jubilee lakini akaangushwa hadi kumaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya mshindi kutoka chama cha ODM na wa pili kutoka UDA.