"Vipi kuhusu mkeo na watoto wako?" Akothee amzomea shemejiye aliyejitoa uhai huku akimuomboleza

"Kwa nini ukawa mbinafsi sana, Odebi? Umevunja mioyo ya watoto wangu,” Akothee aliandika.

Muhtasari

•Akothee alibainisha kuwa uamuzi wa shemejiye umewaacha wengi na mioyo iliyovunjika ikiwa ni pamoja na watoto wake mwenyewe.

•Mama huyo wa watoto watano pia aliomba msamaha kutoka kwa marehemu na kubainisha kuwa wameachwa katika huzuni.

Akothee
Akothee
Image: HISANI

Mwimbaji na mjasiriamali maarufu wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amemwandikia barua ya kihisia marehemu shemeji yake ambaye anadaiwa kujitoa uhai

Katika barua yake, Akothee alimhurumia marehemu shemeji yake lakini akakosoa uamuzi wake wa kujitoa uhai na kuacha familia yake nyuma.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alibainisha kuwa uamuzi wa mwanamume huyo umewaacha wengi na mioyo iliyovunjika ikiwa ni pamoja na watoto wake mwenyewe.

“Mpenzi Shemeji, sina nguvu ya kukuhukumu kutokana na uamuzi ulioufanya wa kumaliza safari hii. Huenda nikataka kuuliza kwa nini hukuwasiliana nami au hata kwa wapwa zako, lakini labda ulifikiri kila mtu alishikwa na matatizo yake,” Akothee aliandika kwenye Instagram.

Aliambatanisha barua yake na picha za kumbukumbu za shemeji yake.

”Lakini sasa, niruhusu nikuulize—vipi kuhusu mke wako na watoto wako? Omuga na wengine? Daudi, je, hukumfikiria mama yako, ambaye amekuwa mjane mwaka mmoja uliopita? Kwa nini ukawa mbinafsi sana, Odebi? Umevunja mioyo ya watoto wangu,” aliongeza.

Akothee alitumia fursa hiyo kufichua kwamba pia yeye amewahi kuwa katika nafasi kama hiyo ambapo afikiri kujitoa uhai lilikuwa chaguo bora zaidi.

Alibainisha kuwa watoto wake walimfanya atupilie mbali mawazo hayo na akaendelea kuhoji kwa nini shemeji yake alifikia hatua ya kukata tamaa.

”Ulikuwa jasiri kutufanyia hivi, ja SDA Unajua ulikuwa kipenzi cha mama zako. Ninaogopa sana kwa ajili ya mama mkwe wetu mgonjwa, "alisema.

Mama huyo wa watoto watano pia aliomba msamaha kutoka kwa marehemu na kubainisha kuwa wameachwa katika huzuni.

“Samahani sana, Odebi. Utusamehe kwa kutokuwepo kwa ajili yako, lakini kusema kweli, sote tumekasirika na maisha haya sasa, sote tunaondoa vichwa vyetu majini ili tu kuepuka kukosa hewa,” Akothee alisema.

"Pumzika kwa amani, Omejo.Yuora ma ok luonga gi nyinga," aliongeza.